Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi Misri inavyorudi Afrika kwa kasi

97786 Misri+pic Jinsi Misri inavyorudi Afrika kwa kasi

Tue, 3 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unapoisikia Misri, mambo yanayokujia harakaharaka kichwani huenda ikawa ni piramidi zinazounda moja ya maajabu saba ya dunia.

Kwa Wakristo wanapoisikia Misri, wanakumbuka kuwa Yesu ambaye alipelekwa nchi hiyo na wazazi wake, Yusufu na Maria akiwa mtoto kukwepa amri ya mfalme wa Kirumi, Herode aliyekuwa ameagiza watoto wote wa kiume wauawe. Yesu alikaa Misri mpaka Herode alipofariki dunia.

Inawezekana kila mmoja akawa na mtazamo wake kuhusu nchi hiyo, lakini jambo la muhimu zaidi ni historia yake ya kuvutia inayowafanya watalii kuitembelea. Habari za mfereji wa Suez na piramidi zinavutia kuona.

Sifa nyingine ni kwamba Misri ni miongoni mwa nchi ambazo watu wake wanajitolea kwa nguvu kuijenga nchi yao. Miradi mbalimbali kama ujenzi wa barabara, majumba na ofisi za Serikali na baadhi ya miradi inafanywa na raia wake na wanachangia gharama zake.

Hata hivyo, kumbukumbu ya maandamano makubwa yaliyofanyika Misri mwaka 2011-2013 na kusababisha mabadiliko ya kisiasa, katiba mpya na siasa mpya zenye mrengo wa wastani, ni suala ambalo bado linakumbukwa na wengi.

Kipindi hicho kilishuhudia kuondolewa madarakani kwa rais aliyedumu kwa miaka 30, Hosni Mubarak na mrithi wake, Mohammed Morsi aliyedumu mwaka moja. Wote wawili sasa ni marehemu, Mubarak akiwa amefariki dunia Februari 25.

Pia Soma

Advertisement
Uchaguzi mkuu ulimuingiza madarakani, Abdel Fattah Al-Sisi ambaye amefanya mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na ushirikiano na nchi nyingine za Afrika na dunia.

Nchi hiyo ambayo ipo barani Afrika ilikuwa ikishirikiana zaidi na nchi za Mashariki ya Kati, lakini tangu utawala wa Al-Sisi imeanza kurudi na kuanza kushirikiana na nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.Rais el-Sisi amekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) kwa mwaka mmoja kuanzia mwaka jana kabla ya kukabidhi kijiti hicho kwa rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa Februari 9.

Kwa kiwango kikubwa, el-Sisi ameirudisha Misri kuwa sehemu ya Afrika si kiramani na mipaka tu kama ilivyoonekana katika tawala nyingine, bali matendo na ushirikiano wa nchi za Jangwa la Sahara.

Ushirikiano wa Misri na nchi nyingine katika sekta mbalimbali kama za kijeshi, usalama, kilimo, viwanda, elimu na miundombinu kwa ujumla ni baadhi ya mambo ambayo yanafanya nchi nyingine za Afrika, kama Tanzania kunufaika.

Kuonyesha kuwa Rais el-Sisi yupo makini na hilo, mwaka 2014 alianzisha taasisi ya ushirikiano ya maendeleo (EAPD) chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri.

Taasisi hiyo, ambayo katibu wake mkuu ni Mahmoud Elmaghraby, imekuwa ikiandaa safari mbalimbali ama kwa Wamisri kwenda nchi nyingine au watu wa mataifa mengine kuingia nchi hiyo kwa lengo la kubadilishana mawazo, maarifa, stadi za maisha na kujionea maendeleo.

Misri ni nchi ambayo ni kama inajengwa upya. Majengo mengi yawe ya Serikali, taasisi binafsi na nyumba za watu binafsi yamebolewa.

“Tunataka kujifunza kutoka kwa mataifa mengine, lakini pia tunataka kujifunza kutoka kwao, mpo hapa kwa ajili ya kubadilishana uzoefu,” anasema Elmaghraby akiwakaribisha wahariri 20 wa vyombo vya habari kutoka nchi za Afrika waliokuwa na ziara maalumu ya siku kumi.

Jambo ambalo raia wa Misri yenye watu milioni 104 wanaweza kujivunia ni jinsi wanavyojitoa kwa ajili yao na ndio maana utashangaa unaposikia wanajenga mji mpya wa Cairo ambao utakuwa makao makuu mapya pamoja na mradi mkubwa wa kuongeza mfereji wa Suez maarufu kama Suez Canal.

Katika historia tunajifunza kuwa mrefeji wa Suez ulijengwa kwa jasho na damu, huku watu wengi wakifariki dunia kabla ya kuzinduliwa rasmi Novemba 17, 1869 na katika kipindi hicho ulikuwa ukifungwa na kufunguliwa zaidi ya mara tano kwa sababu mbalimbali.

Mfereji huo unaunganisha bahari ya Mediterean na bahari ya Shamu (Red Sea) na sasa unatambuliwa kama nembo ya uhuru wa watu wa Misri, kwa kuwa licha ya kuunganisha nchi hiyo na nchi nyingine za Mashariki ya Kati, mateso na vifo vya walioshuturutishwa kujenga mfereji huo katika karne ya 17 bado vipo katika kumbukumbu za wengi.

Mkuu wa mamlaka ya mfereji wa Suez, Osama Rabie anasema kutokana na kupanuka kwa biashara na mataifa mbalimbali, Misri imetanua na kujenga mfereji mpya wa Suez kwa kuuongezea urefu na upana, hivyo kufanya meli nyingi zaidi kuingia. Meli zilizokuwa zinasubiri kwaa saa 22 kabla ya kushusha mizigo, sasa zinatumia saa 11 tu.

Anasema faida ambazo nchi hiyo imepata kutokana na ujenzi mpya wa mfereji huo ni kuongeza shehena za kontena na kuongeza idadi ya meli kutoka 49 mpaka 97 kwa siku.

“Ilichofanya serikali ni kuwatangazia wananchi mpango wa kuongeza ukubwa wa mfereji huo na wakaomba kila mwananchi kuchangia katika akaunti maalumu ya benki,” anasema.

“Jambo la kushangaza ni kuwa benki zilifurika watu kuanzia maskini mpaka matajiri na wote walijitolea kuchangia jumla ya pauni 20 bilioni ambazo zimejenga mfereji mpya bila kutumia fedha nyingine ya msaada.”

Kujitokea kwa watu hao hakukushangaza na ndio maana tangu mradi huo utangazwe Agosti 4, 2014 ilishuhudia mradi huo wenye urefu wa kilometa 72 ukikamilika kwa mwaka mmoja tu mpaka Agosti 6, 2015.

Mfereji huo sasa upo chini ya Mamlaka ya Mfereji wa Suez ambayo inasimamia kila kitu kuanzia chuo cha mabaharia na marubani.

Jambo jingine ambalo wanalifanya kwa nguvu sasa, ni kujenga mji mpya wa Cairo wenye wakazi milioni 20 ambao wanaamini utapunguza changamoto nyingi.

Kwa miaka 40, Misri imekuwa inafikiria kuwa na mji mpya, lakini ndoto hiyo sasa imefika ukingoni kutokana na ujenzi huo.

Misri inakuwa miongoni mwa nchi 30 duniani zilizohamishia makao makuu yake kwenda miji mingine, lakini tofauti ni kwamba mji huo Cairo hiyo ‘mpya’ iliyopo mita 45 kutoka mji wa sasa, inajengwa kuanzia hatua za mwanzo kwa sababu hakukuwa na jengo lolote awali.

Mji huo ambao unakaribia kukamilika, utakuwa na Ikulu, jengo la bunge, benki kuu, wizara zote, ofisi za wilaya, uwanja wa kisasa wa ndege pamoja na nyumba ambazo zitachukua watu milioni 6.5.

Ingawa bado haujapewa jina zaidi ya kuitwa makao makuu mapya, unajengwa kwa hatua. Hatua ya mwanzo ikiwa ni kuhakikisha ofisi za Serikali na nyumba za watumishi zinakamilika mapema huku utaratibu ukiwekwa wa mabasi kusafirisha watu kutoka Cairo ya sasa.

Mji huo ulioanza kujengwa Mei 2016, na sasa umekamilika baadhi ya majengo na ndio maana haikuwa ajabu kwa Rais el-Sisi kuzindua kanisa kubwa kuliko yote linaloitwa “Uzao wa Kristo” pamoja na msikiti mkubwa wa kisasa unaoitwa Al-Fattah-Al-Aleem. Ni msikiti wa pili kwa ukubwa baada ya ule wa Mecca, saudi Arabia.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa rais huyo kuingia au kutembelea kanisa ukiacha rais wa mpito, Adly Mansour ambaye alitembelea kanisa la Orthodox wakati wa sherehe za Krismasi mwaka 2013. Hata Hosni Mubaraka aliyetawala kuanzia 1981 mpaka 2011 hajawahi kufanya kitendo hicho.

Mradi huo ambao uko kilomita nane kutoka mfereji wa Suez, unakadiriwa kugharimu dola 3 bilioni kabla ya kukamilika mwaka 2023.

Sehemu inayovutia zaidi ni katika piramidi ambazo inasadikiwa kuwa yalikuwa ni makaburi walikozikwa wafalme, vongozi wa dini na watu mbalimbali. Inadaiwa kuna zaidi ya piramidi 100 katika nchi hiyo.

Hata hivyo, piramidi maarufu zaidi ni zile zilizopo maeneo ya Giza, nje kidogo ya jiji la Cairo. Inadhaminiwa kuwa ni piramidi kubwa zaidi kuwahi kutokea. Piramidi la Khufu lililopo Giza ndio kubwa zaidi kuliko yote Misri, na ni miongoni mwa maajabu saba ya dunia.

Maeneo hayo ya Giza ambako yamekuwa yakifurika watu, hasa Ijumaa na Jumamosi ambazo ni siku za mapumziko Misri. Jumapili ni siku ya kazi.

Unapofika maeneo hayo ya Giza unapaswa kuwa makini kwa sababu utakutana na vijana wanaotaka kukupiga picha pamoja na ngamia wao na wakati mwingine watakwambia upande ngamia na kisha ulipe na kama huna fedha, jasho litakutoka, kwa kuwa humfanya ngamia asilale ili uweze kushuka. Pia usikubali kupewa kitu cha bure unapokuwa maeneo hayo.

Misri ni miongoni mwa nchi zinazofuata maadili ya dini ya Kiislamu, kuna kituo cha Al Azhar ambacho ni taasisi maarufu zaidi ya Kiislamu duniani yenye msikiti mkubwa na yenye chuo kikuu.

Al Azhar ina taasisi za elimu ambazo pia zinafundisha maadili mema na kuhakikisha vijana hawajiungi na vikundi vya kigaidi.

Dk Ahmed Al-Tayyib, ambaye ni imamu mkuu wa msikiti huo mkubwa kuliko yote Misri, anasema taasisi hizo zinatoa elimu ya uhandisi, utabibu na kozi nyingine zipo chini ya mwavuli wa Al Azhar.

Al-Azhar imetoa wasomi katika zama zote na sifa mojawapo ni kukuza harakati za kifikra kwa ujumla na hasa kifasihi na kati ya wataalamu na viongozi wa kifikra wa taasisi hiyo ni imamu na sheikh mkuu wa Al Azhar, Dk Ahmed Al-Tayyib ambaye amekuwa na nafasi hiyo tangu Machi 19, 2010.

Taasisi hiyo inatoa pia huduma na kozi za tiba, uhandisi, zahanati, sayansi ya hisabati, fizikia, kemia, baiolojia, kilimo na jiolojia na jambo la kushangaza zaidi ni kitivo cha Kiswahili ambacho kinafundisha lugha hiyo tu.

Miaka yote walikuwa wakitoa ufadhili kwa wanafunzi 800 kwa mataifa mengine ya Afrika, lakini mwaka jana walitoa kwa wanafunzi zaidi ya 1,600 kumuunga mkono rais wao, el-Sisi aliyekuwa mwenyekiti wa AU mpaka Februari mwaka huu.

Dk Al-Tayyib anasema licha ya kutoa walimu kwenda kufundisha nchi nyingine za Afrika, wanalenga kuhakikisha bara hili linakuwa na amani na usalama ndio maana wanafundisha vijana jinsi ya kujiepusha na ugaidi.

Suala hilo pia linasisitizwa na papa wa makanisa ya Orthodox yenye wafuasi milioni 15 nchini Misri ambaye anaelezea umuhimu wa makanisa yake katika kujenga umoja, ushirikiano na mataifa mengine duniani.

Uwekezaji wa elimu ni jambo kubwa. Kuna vyuo kutoka mataifa mengine ambavyo vina ubora wa hali ya juu, mmojawapo ikiwa ni Chuo Kikuu cha Ujerumani cha jijini Cairo ambacho kimejikita katika uhandisi, teknolojia na utabibu. Mitambo ya teknolojia ya kisasa ambayo inapatikana katika chuo hicho ni ya hali ya juu.

Chuo kingine ni chuo kikuu cha Uingereza ambacho pia huchukua wanafunzi kutoka nchi za Afrika.

Katika vituo vya kijeshi, kama chuo cha mafunzo ya juu ya kijeshi na kwenye chuo cha polisi, wanafunzi wanapata mafunzo ya darasani, lakini pia wanaonekana wakifanya mazoezi ya hali ya juu kukabiliana na mambo mbalimbali.

Chanzo: mwananchi.co.tz