Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jinsi Afrika inavyopambana na ukiritimba wa nje

Ukiritimba Afrika.jpeg Jinsi Afrika inavyopambana na ukiritimba wa nje

Tue, 11 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya Mali na Burkina Faso kuwafukuza mabalozi wa Ufaransa, majuzi Chad ilimpa balozi wa Ujerumani muda wa masaa 48 kuwa ameondoka nchini humo.

Wizara ya Habari na Mawasiliano ya Chad ilitangaza uamuzi huu juzi ikisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na "mtazamo wake usio na adabu" na "kutoheshimu kanuni za kidiplomasia."

Balozi wa Ujerumani nchini Chad, Jan Christian Gordon Kricke, hivi karibuni aliingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo na kukosoa kucheleweshwa zoezi la uchaguzi wa Chad. Balozi wa Ujerumani alikuwa tayari ameonywa mara kadhaa kuhusu kauli zake za kuingilia mambo ya ndani ya Chad.

Chad inakuwa nchi ya tatu barani Afrika baada ya Burkina Faso na Mali kumfukuza balozi wa nchi ya Ulaya. Hapo awali, Burkina Faso na Mali ziliwatimua mabalozi wa Ufaransa na kuonya dhidi ya uingiliaji kati wa nchi za Magharibi katika masuala ya barani Afrika.

Katika miezi ya hivi karibuni mivutano ya kisiasa kati ya nchi za Afrika na nchi za Magharibi hususan Ufaransa na Ujerumani, imeongezeka.

Ijapokuwa nchi za Magharibi zimekuwepo katika baadhi ya nchi za Kiafrika kwa miongo kadhaa kwa visingizio mbalimbali kama madai ya kusaidia juhudi za kuimarisha usalama au kupambana na ugaidi, lakini kuzuka kwa vita vya Ukraine na haja ya nchi za Magharibi ya kuendeleza uhusiano wao na Afrika vimebadili mtazamo wa Wamagharibi.

Kwa upande mwingine, kutofanikiwa kwa nchi za Magharibi ikiwemo Ufaransa katika kupambana na magenge ya waasi nchini Mali kumezifanya nchi nyingi za Kiafrika kutaka kusitishwa uingiliaji wa nchi za Magharibi katika masuala ya Afrika. Mota Muhammad Ali, mchambuzi wa masuala ya kisiasa ya Afrika, amedokeza kuwa nchi za bara hilo zinajaribu kupunguza utegemezi wao kwa nchi za Magharibi na kusema: Nchi za Kiafrika zinajaribu kuwa huru zaidi ikilinganishwa na huko nyuma, ili zisikoloniwe tena na nchi za Magharibi kama ilivyokuwa hapo awali. Zinataka kuzionyesha nchi nyingine duniani kwamba mashinikizo ya Magharibi hayawezi kuzilazimisha nchi za Kiafrika kutekeleza matakwa yao kama zilivyofanya katika miaka 10 au 20 iliyopita.

Ukweli ni kwamba, nchi za Kiafrika haziko tayari tena kukubali udhibiti na ukiritimba wa Wamagharibi, katika zama hizi za mabadiliko ya kisiasa katika uga wa kimataifa, kupanda kwa viwango vya elimu na ufahamu, na kuibuka kwa kizazi kipya cha viongozi wenye mwamko na ghera ya mataifa yao. Viongozi wa kizazi kipya cha Afrika wanajaribu kufanya maamuzi yao wenyewe kwa kupanga sera na siasa zenye maslahi kwa mataifa ya Afrika na kupanua uhusiano na ushirikiano na madola yanayoinukia kisiasa na kiuchumi.

Kwa sasa nchi nyingi za Kiafrika zina uhusiano mkubwa na China, India, Brazil au Russia. Nchi hizi sio tu zimekuwa washirika wakuu wa kibiashara wa nchi za bara la Afrika, lakini pia katika suala la usalama, nchi za Kiafrika zinajielekeza upande wa kuwa na washirika mseto kwenye sekta hii.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavrov, anasema: Marekani na nchi za Ulaya, ambazo zinataka kusitisha ushirikiano wa nchi za Kiafrika na Russia, kwa hakika zinataka kurejesha utegemezi wa kikoloni wa Magharibi kwa nchi za Afrika.

Kufukuzwa balozi wa Ujerumani nchini Chad kunaweza pia kutathminiwa kuwa ni katika juhudi za kupunguza ushawishi wa nchi za Ulaya barani Afrika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live