Wakati mapigano makali ya silaha yakiendelea katika miji mbalimbali ya Sudan kwa mwezi wa nne, Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imetaja sharti la jeshi kurejea kwenye mazungumzo ya amani.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema kuwa kuondoka kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwenye makazi ya raia ndio sharti kuu la jeshi kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Jeshi la Sudan linawatuhumu wapiganaji wa RSF kuwa wanawatumia raia kama ngao za kujihami katika vita, suala ambalo Vikosi vya Msaada wa Haraka vinasema, ni tuhuma zisizo na masingi.
Sambamba na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Sudan na RSF, machafuko ya kikabila pia yanaripotiwa kupamba moto huko Darfur, jambo ambalo linatatiza hali ya mambo nchini Sudan.
Hapo awali, televisheni ya Al Jazeera ya Qatar ilitangaza kuwa ghasia za kikabila katika jimbo la Darfur Kusini zimesababisha vifo vya watu 120 katika siku mbili zilizopita.
Mapigano makali yaliyozuka tarehe 15 Aprili 2023 baina ya majenerali wa jeshi huko Sudan yameshasababisha vifo vya maelfu ya raia, huku mamilioni ya wengine wakilazimika kuyahama makazi yao.