Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jeshi la Sudan lasema litakabidhi madaraka kwa wafuasi wake pekee

Jeshi La Sudan Lasema Litakabidhi Madaraka Kwa Wafuasi Wake Pekee Jeshi la Sudan lasema litakabidhi madaraka kwa wafuasi wake pekee

Thu, 11 Apr 2024 Chanzo: Bbc

Kiongozi wa kijeshi wa Sudan Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan amesema jeshi "halitakabidhi mamlaka ya taifa letu kwa chama chochote cha ndani au nje".

"Yeyote aliyepanga njama dhidi ya watu wa Sudan ndani na nje ya nchi hatakuwa na jukumu lolote katika uendeshaji wa siku zijazo wa nchi hii," Jenerali Burhan alisema alipokuwa akiwahutubia waumini baada ya sala ya Eid al-Fitr katika msikiti mmoja katika jimbo la Gedaref la kati.

Pia alisisitiza kwamba "jimbo litaendeshwa na wale tu ambao wamesimama kidete dhidi ya udhalimu na ukiukaji wa haki," shirika la habari la serikali la Suna liliripoti.

Kiongozi huyo wa kijeshi alionya kwamba hakutakuwa na mazungumzo yoyote kuhusu kurejea kwa utawala wa kidemokrasia hadi pale mzozo uliozuka Aprili 2023 utakapomalizika.

Jeshi limepata uungwaji mkono kutoka kwa vyama vya Kiislamu ambavyo vilikuwa na ushawishi mkubwa wakati wa uongozi wa muda mrefu wa Omar al-Bashir ambaye aliondolewa madarakani Aprili 2019.

Mazungumzo kati ya jeshi la Sudan na Rapid Support Forces yanayopatanishwa na Marekani na Saudi Arabia yalitarajiwa kurejelewa huko Jeddah baada ya Eid.

Katika ujumbe wa sauti kwenye akaunti yake ya mtandao wa X kuadhimisha Eid al-Fitr, kiongozi wa RSF Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti, alisema kwamba "hakuna chaguo jingine kwa Rapid Support Forces isipokuwa ushindi tu".

Hemedti pia aliahidi kumfungulia mashitaka mwanajeshi yeyote atakayefanya ukiukwaji wa haki dhidi ya raia wasio na hatia na kuviagiza vikosi vyake kutomvumilia mhalifu yeyote anayetishia utulivu wa wananchi.

Chanzo: Bbc