Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) limekomboa vijiji vinne, ambavyo vilikuwa ngome za genge la kigaidi la al Shabab katika eneo la kusini-magharibi mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Wizara ya Ulinzi ya Somalia imesema kwenye taarifa yake iliyoripotiwa jana kwamba, wanajeshi wa nchi hiyo wamechukua udhibiti wa vijiji vya Dudumale, Bulo-Kajor, Abagbeday na Elgaras katika mji wa Hudur baada ya mashambulizi yaliyoashiria kuanza awamu ya pili ya kampeni ya serikali ya kupambana na magaidi wakufurishaji wa al Shabab.
Sehemu moja ya taarifa hiyo iliyotolewa Moghadishu, mji mkuu wa nchi hiyo imesema: "Jeshi la Taifa la Somalia limechukua udhibiti wa vijiji vilivyokuwa vinakaliwa kwa mabavu na Khawarij (ikikusudia al Shabab)."
Taarifa hiyo pia imesema: "Huu ni mwanzo wa awamu ya pili na hatua madhubuti ya kurejesha usalama kwa jamii zetu." Magaidi wa al Shabab wanazidi kufurushwa
Wizara hiyo vilevile imesema kuwa, vikosi vya serikali vimerejesha amani na usalama katika vijiji vilivyokombolewa ambako magaidi wa al Shabab walikuwa wamejificha na kuwatia hofu wananchi wa eneo hilo.
Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) na washirika wake kwa sasa wanashiriki katika operesheni za pamoja za kijeshi dhidi ya genge la kigaidi la al Shabab baada ya kukamilika awamu ya kwanza ambayo ilikomboa maeneo ya kati na kusini mwa Somalia yaliyokuwa chini ya udhibiti wa magaidi hao.
Mwanzoni mwa mwezi ulioisha wa Oktoba, serikali ya Somalia ilitangaza kuwa, imefanikiwa kuangamiza wanachama 1,650 wa genge la kigaidi la al Shabab katika operesheni za vikosi vya jeshi la nchi hiyo kwenye kipindi cha miezi miwili.
Shirika rasmi la habari la Somalia (SONNA) lilitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, makamanda 19 wa ngazi za juu wa al Shabab ni miongoni mwa mamia ya wanachama wa genge hilo walioangamizwa katika operesheni hizo.