Wanajeshi waliofanya mapinduzi dhidi ya utawala wa ukoo wa Bongo uliogawala Gabon kwa miaka 55 wameamua kufungua mipaka ya nchi hiyo kutokana na hali kuendelea kuwa shwari.
Jenerali Brice Oligui Nguema, alitangazwa siku ya Jumatano kuwa mkuu wa serikali ya mpito ya nchi hiyo.
Jenerali Nguema ambaye alikuwa mkuu wa walinzi wa rais, siku ya Jumatano aliongoza maafisa wa kijeshi kufanya mapinduzi yaliyomng'oa madarkani Rais Ali Bongo Ondimba na kukhitimisha miaka 55 ya utawala wa ukoo wa Bongo katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.
Rais Ali Bongo, 64, aliong'olewa madarakani siku chache baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa mwishoni mwa juma matokeo ambayo wapinzani waliyalalamikia vikali na kusema ulikuwa ni udanganyifu mtupu.
Rais Ali Bongo aliyepinduliwa na wanajeshi siku ya Jumatano
Majenerali waliofanya mapinduzi ya kijeshi huko Gabon walisema wamevunja taasisi zote za serikali na wamefuta pia matokeo ya uchaguzi pamoja na kufunga mipaka. Kesho Jumatatu Jenerali Brice Oligui Nguema anatarajiwa kuapishwa kuwa rais wa serikali ya mpito ya Gabon.
Mipaka ya Gabon imefunguliwa baada ya kuripotiwa kuwa, maisha yameanza kurejea katika hali ya kawaida nchini humo siku chache baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyompindua Rais Ali Bongo na baada ya kiongozi wa kipindi cha mpito kuahidi kurejesha utawala wa Katiba nchini humo.
Hali ya utulivu iliripotiwa kutanda Ijumaa na Jumamosi katika mitaa ya mji mkuu Libreville. Mashirika ya serikali yameanza tena kufanya kazi, na jeshi limeondoka katika mitaa, ingawa bado linasimamia baadhi ya vituo vya ukaguzi.
Jeshi la Gabon linasema limefanya mapinduzi kwa sababu ya kuchakachuliwa matokeo ya uchaguzi, na kwamba serikali ya Ali Bongo ilitawaliwa na rushwa na kutowajibika.