Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jeshi la DRC latangaza kuzuia jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Felix Tshisekedi

Jeshi La DRC Latangaza Kuzuia Jaribio La Mapinduzi Dhidi Ya Rais Felix Tshisekedi Jeshi la DRC latangaza kuzuia jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Felix Tshisekedi

Sun, 19 May 2024 Chanzo: Bbc

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuwa limezuia jaribio la mapinduzi dhidi ya Rais Felix Tshikedi huko Kinshasa.

Msemaji wa jeshi la DR Congo Brig Jenerali Sylavin Ekenge amesema kwenye kituo cha runinga cha taifa RTNC TV kwamba washukiwa kadhaa wanazuiliwa na "hali sasa imedhibitiwa".

Tangazo hili liinajiri saa chache baada ya watu wenye silaha kushambulia nyumba ya Vital Kamerhe, mkuu wa zamani wa majeshi na mshirika wa karibu wa Rais Felix Tshisekedi Jumapili asubuhi.

Walioshuhudia wanasema kundi la takriban washambuliaji 20 wakiwa wamevalia sare za jeshi walishambulia makazi hayo na ufyatulianaji wa risasi ukafuatia.

Ripoti za vyombo vya habari vya ndani zilisema washambuliaji hao walikuwa wanachama wa Vuguvugu la New Zaire linalohusishwa na aliyekuwa mwanasiasa aliyeko uhamishoni Christian Malanga.

Walinzi wawili na mshambuliaji waliuawa katika shambulio la nyumba ya Bw Kamerhe, msemaji wake na ubalozi wa Japan umeandika kwenye machapisho ya mtandao wa kijamii wa X.

BBC imeona video ya Bw Malanga akisema kwa Kilingala, lugha ya wenyeji: "Sisi wanajeshi tumechoka, hatuwezi kuandamana pamoja na Vital Kamerhe na Rais FĂ©lix Tshisekedi."

Rais Tshisekedi alichaguliwa tena kwa muhula wa pili katika uchaguzi uliozozaniwa mwaka jana mwezi Disemba.

Alishinda takriban 78% ya kura. Takriban watu 20 waliuawa katika ghasia zinazohusiana na uchaguzi wakati wa maandalizi ya upigaji kura.

Kongo ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini na idadi kubwa ya watu, lakini licha ya hali hii maisha hayajaboreka kwa watu wengi, huku migogoro, ufisadi na utawala mbovu vikiendelea.

Sehemu kubwa ya maliasili za nchi hiyo ziko mashariki ambako ghasia bado zinaendelea licha ya jitihada za Bw Tshisekedi za kukabiliana na hali hiyo na kuleta wanajeshi wa kikanda.

Rais Tshisekedi hajatoa tamko lolote kuhusu tukio hili kufikia muda wa machapisho.

Balozi wa Japani katika mji mkuu wa Kongo amewaonya wajapani walioko DRC kutotoka nje.

Chanzo: Bbc