Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jeshi la Cameroon laua wapiganaji watano wanaotaka kujitenga

Cameroon Jeshi Jeshi la Cameroon laua wapiganaji watano wanaotaka kujitenga

Thu, 11 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Takriban wapiganaji watano wanaotaka kujitenga wameuawa katika shambulizi lililofanywa na jeshi la Cameroon dhidi ya watu hao waliokuwa wamejizatiti kwa silaha katika eneo la Kaskazini-Magharibi mwa nchi hiyo linalozungumza Kiingereza.

Duru mbalimbali za habari zimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, shambulio hilo lilitokea Jumanne katika kijiji cha Ewai cha kaskazini magharibi mwa Cameroon.

Afisa mmoja wa jeshi amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, wanajeshi wa Cameroon walivamia maficho ya watu hao wanaotaka kujitenga, ambayo yalikuwa kama kituo kikuu cha moja ya vikundi vinavyotaka kujitenga katika eneo hilo, na kuua wapiganaji watano.

Afisa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa madai kwamba si msemaji rasmi ameongeza kuwa: "Wanajeshi wetu jasiri wamekamata pia silaha nyingi na kuokoa baadhi ya watu waliotekwa nyara na magaidi hao wanaotaka kujitenga. Wengi wa magaidi hao walitoroka wakiwa na majeraha ya risasi." Maeneo yanayotaka kujitenga nchini Cameroon

Hata viongozi wa makundi ya wanaotaka kujitenga wamethibitisha kutokea shambulio hilo kwenye mitandao ya kijamii lakini wamedai kuwa ni wapiganaji watatu pekee ndio waliouawa.

Mkazi wa kijiji hicho ambaye naye hakutaka jina lake litajwe, amesema kuwa, mamia ya watu katika kijiji hicho walikimbilia msituni wakati mashambulizi hayo yalipokuwa yanaendelea.

Jeshi la Cameroon halikusema kwa upande wake limepata hasara kiasi gani katika makabiliano hayo ya silaha kama ambavyo haikusema chochote pia kuhusu wanajeshi wake waliojeruhiwa.

Maeneo yanayozungumza Kiingereza ya kaskazini magharibi mwa Cameroon yamekuwa yakipigania kujitenga kwa miaka mingi sana. Mgogoro baina yao uliingia kasi mwaka 2017 wakati vita vya silaha viliposhadidi baina yao na jeshi la serikali. Maeneo hayo yanataka kuanzisha taifa huru katika mikoa miwili inayozungumza Kiingereza ya kaskazini magharibi na kusini magharibi mwa Cameroon, suala ambalo linapingwa vikali na serikali ya nchi hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live