Jitihada za Afrika Kusini kutaka ndugu wawili wa familia tajiri ya Gupta kurejeshwa kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimeshindikana.
Atul na Rajesh Gupta wanashutumiwa nchini Afrika Kusini kwa kufaidika na uhusiano wao wa karibu na Rais wa zamani Jacob Zuma na kuwa na ushawishi usio wa haki.
Wizara ya sheria ilisema imefahamu kwa "mshtuko na kufadhaika" kuhusu hatua hiyo.
Ndugu hao wanaokana kosa lolote, walitoroka baada ya tume ya mahakama kuanza kuchunguza kashfa kubwa ya ufisadi.
Gupta wazaliwa wa India walikamatwa katika UAE Juni mwaka jana na mazungumzo ya kuwarejesha nchini Afrika Kusini yalianza.
Lakini mahakama katika Umoja wa Falme za Kiarabu ilikataa ombi la kurejeshwa nchini kwa sababu ya kiufundi, tovuti ya habari ya TimesLive inamnukuu Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini Ronald Lamola akisema.
Uamuzi huo ulifanywa mwezi Februari lakini ulifikishwa tu kwa Afrika Kusini siku ya Alhamisi.
"Sababu zilizotolewa za kukataa ombi letu hazielezeki na zinatokana na uhakikisho uliotolewa na mamlaka ya Imarati kwamba maombi yetu yanakidhi matakwa yao," Bw Lamola alisema, Mail & Guardian ya Afrika Kusini inaripoti.
Mahakama ya UAE ilikuwa imeamua kwamba kwa vile kulikuwa na makosa ya utakatishaji fedha yanayodaiwa kufanywa katika UAE na Afrika Kusini basi UAE ilikuwa na mamlaka ya kuwafungulia mashitaka wana Gupta, Reuters inamnukuu waziri huyo akisema.
Bw Lamola alisema serikali yake itakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Katika wiki za hivi karibuni kumekuwa na ripoti za vyombo vya habari kwamba ndugu hao hawakuwa tena kizuizini na wameonekana nchini Uswisi.
Wizara ya haki haikuweza kuthibitisha hilo au ikiwa ndugu, ambao walikuwa wamepewa uraia wa Afrika Kusini, walikuwa wamepata hati za kusafiria kutoka katika kisiwa cha Vanuatu, kisiwa cha Pasifiki.