Mlinzi wa usalama amempiga risasi na kumjeruhi mwanaume mmoja ambaye alikuwa amavaa sare ya kijeshi nje ya ubalozi wa Urusi katika mji mkuu Harare, Jumatano usiku, polisi imesema.
Msemaji wa polisi Paul Nyathi ameiambia BBC kuwa mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 24 alikuwa amekabiliana na walinzi wa usalama katika ubalozi huo.
Alipelekwa katika hospitali yae neo hilo ambako ameendelea kushikiliwa huku polisi wakiendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Afisa habari katika ubalozi wa Urusi , Egor Kuropitnik, ameiambia BBC kuwa picha za uchunguzi zilionyesha kuwa mwanaume huyo alikuwa akitembea kuelekea walipokuwa walinzi.
Wakati alipokaribia ukuta wa ubalozi ofisa alifyatua kile ambachio kingekuwa ni risasi ya tahadhari, lakini mwanaume huyo aliendelea kusonga mbele kuelekea eneo la usalama. Risasi ya pili ilifyatuliwa na mwanaume akaanguka.
Hakuonekana kwamba alikuwa anajaribu kupanda ukuta wa uzio wa ubalozi, Bw Kuropitnik alisema.