Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jamaa alivyopanga kifo cahke kwa miaka saba

Kifo Ns Jamaa alivyopanga kifo cahke kwa miaka saba

Sun, 15 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwalimu kutoka Kaunti ya Nyeri aliyepatikana akiwa amefariki nyumbani kwake katika kijiji cha Ihururu, Alhamisi, alianza kupanga kuhusu kifo chake miaka saba iliyopita, ‘Taifa Jumapili’ imebaini.

Mnamo Alhamisi, mwili wa Bw Joseph Gathogo ulipatikana katika sebule ya nyumba yake ya kukodisha yenye vyumba viwili ukiwa umewekwa kwenye jeneza.

Alikuwa amekosekana kwa muda wa wiki tatu tangu Desemba 23, baada ya kusimamia Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) katika Shule ya Upili ya Muhoya, alikokuwa akifanya kazi.

Wakiwahutubia wanahabari mnamo Jumamosi, marafiki na majirani waliotagusana na marehemu walifichua vile alianza kukusanya vifaa vya kutengeneza kaburi lake lenye umbo la boti na jeneza lenye urefu wa futi tatu.

Mnamo 2017, mwenye nyumba alimokuwa akikaa, Bw Daniel Kiama, alisema alikata mti ili kuuza mbao.

Wakati huo, Bw Gathogo aliomba mbao kadhaa akidai alikuwa akitengeneza sanduku la kuwekea nguo. Marehemu alikuwa mwalimu wa masomo ya Bayolojia na Tarakilishi katika Shule ya Upili ya Muhoya.

“Alimwambia mamangu (marehemu) kwamba nguo zake zilikuwa zikipata uchafu, hivyo alihitaji mahali pazuri pa kuziweka,” akasema.

Hata hivyo, hakumwona akitengeneza sanduku hilo, kwani aliingiza mbao hizo katika nyumba yake, ambayo ilikuwa imefungwa kila wakati.

Mwaka 2022, alimuuliza mmoja wa majirani wake mahali ambapo angenunua mfuko mmoja wa simiti.

Jirani na rafiki yake wa karibu ambao hawakutaka kutajwa walisema walimwelekeza marehemu, 44, kwa duka la karibu.

Baadaye, aliitumia simiti hiyo kutengeneza kaburi lenye umbo la boti.

Kulingana na mwenye nyumba hizo, marehemu hakuwa akiwakaribisha wageni wowote, wala hakuwahi kuonekana na mwanamke yeyote kwa muda wa miaka 19 aliyokaa kama mpangaji.

“Ikiwa ulimhitaji, angekupigia simu badala ya kwenda katika nyumba yake,” akasema, akiongeza kuwa marehemu alijulikana kama mtaalamu wa kompyuta, kwani alikuwa akiwatengenezea vifaa hivyo kila mara vilipoharibika.

“Hata kwa wateja wake, alikuwa akiwaambia kuacha tarakilishi zao au simu katika eneo fulani, ambako angezichukua na kuzirudisha baada ya kuzitengeneza,” akasema.

Majirani wake wanamtaja kuwa msiri kwani hakuzungumza kuhusu maisha yake ya kibinafsi, ijapokuwa alipenda kandanda, muziki wa zamani na siasa.

“Alikuwa shabiki mkubwa wa timu ya Arsenal na alipenda historia, hasa ya Misri Kongwe na jamii ya Agikuyu,” akasema jirani ambaye hakutaka kutajwa, akiongeza kuwa mijadala kama hiyo ilimchangamsha pakubwa hata hadharani, licha ya sifa yake ya kutotaka kuingiliana na watu.

Huku polisi wakiendelea kubaini sababu yake kujitoa uhai, majirani wanadai huenda marehemu alikuwa akifuata tamaduni za kizamani kutoka vitabu vinavyoangazia maisha na tamaduni za Misri.

Marehemu aliripotiwa kupotea kwa polisi na familia yake inayoishi katika eneo la Ngangarithi, mjini Nyeri mnamo Januari 7.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live