Baada ya kesi kusikilizwa na mahakama siku ya Alhamisi, jaji aliamuru kiongozi wa upinzani wa Senegal Ousmane Sonko arejeshwe kwenye orodha ya wapiga kura.
Jina la Bw Sonko liliondolewa kwenye orodha ya waliostahili kupiga kura baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela mwezi Agosti.
Alipatikana kuwa alitenda kinyume cha maadili kwa mtu mwenye umri wa chini ya miaka 21, lakini alikanusha madai hayo, akisema kuwa kesi hiyo ilichochewa kisiasa.
Mawakili wa Bw Sonko walisema uamuzi wa jaji huyo Alhamisi ulimfungulia njia ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa urais utakaofanyika Februari mwaka ujao. Hata hivyo, hii haijathibitishwa.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa Ijumaa, mawakili wa serikali walisema watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Kesi hiyo ilisikilizwa katika mahakama ya Ziguinchor, mji wa kusini ambapo Bw Sonko alikuwa kwenye orodha ya wapiga kura, na ambapo yeye ni meya.
Hukumu yake ya "kupotosha vijana" ilizua maandamano ya ghasia katika mojawapo ya mataifa ya Afrika yenye utulivu. Takriban watu 16 walifariki na mamia kujeruhiwa, kulingana na maafisa.
Mwishoni mwa Julai, kiongozi wa upinzani alifungwa kwa mashtaka mapya: kutoa wito wa uasi, njama ya uhalifu kuhusiana na biashara ya kigaidi na kuhatarisha usalama wa serikali.
Aliyekuwa mtumishi wa umma, Bw Sonko alipata umaarufu katika uchaguzi wa urais wa 2019, ambapo aliibuka wa tatu.