Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jaji akutwa amekufa

88873 Jaji+pic Jaji akutwa amekufa

Wed, 18 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kisumu, Kenya. Jaji wa Makahama ya Rufaa, Profesa Otieno Odek amefariki dunia ghafla.

Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisumu, Julius Ng’arng’ar alisema Jaji Odek alikumbwa na umauti jana asubuhi nyumbani kwake umbali wa mita 50 kutoka kituo kikuu cha Polisi cha Kisumu.

Kifo cha Profesa Odek kimekuja siku chache baada ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Noordin Haji kumtaka akatoe ushahidi dhidi ya kesi ya rushwa inayomkabili Wakili Tom Ojienda.

Akizungumzia kifo hicho, Hakimu Ng’arng’ar alisema sababu za kifo cha jaji huyo hazijafahamika.

Alisema tayari Jeshi la Polisi nchini Kenya limeanza uchunguzi kuhusu kifo hicho. “Kwa sasa mwili umehamishwa katika Hospitali ya Aga Khan, Kisumu kwa taratibu zaidi za uchunguzi, alisema.

Hakimu Ng’arng’ar alisema Profesa Odek alionekana mara ya mwisho Ijumaa iliyopita na tangu wakati huo alikuwa hapokei simu yake ya kiganjani. “Hakuwa akijibu simu zilizomtaka kuripoti kazini wakati alipotafutwa asubuhi baada ya kushindwa kutokea ofisini kama kawaida yake.”

Dereva wa jaji huyo alipoulizwa kuhusu kifo cha bosi wake alisema alifika nyumbani kwake asubuhi kumchukua kama kawaida na kumsubiri nje, lakini hakutokea.

Polisi nchini humo ilisema kuwa baada ya taarifa ya kutoonekana kwa jaji huyo walifika nyumbani kwake na kuvunja moja ya dirisha lake la kioo. “Tulipoingia tukakuta televisheni imewashwa na simu za jaji zilikuwa mezani.

“Alikuwa amefunikwa kawaida kama mtu anayelala,” ilisema sehemu ya taarifa ya jeshi hilo la polisi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa hakukuwa na mapambano yoyote kabla ya umauti kumkuta Profesa Odek.

“Tutatoa taarifa kamili baada ya muda mfupi, watu wawe watulivu,” ilisema taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na familia ya kiongozi huyo.

“Hakuwa jaji pekee, lakini tumepoteza msomi mzuri wa sheria, kifo chake kimeshangaza sana,” alisema Jaji Maranga.

Mtu mwingine aliyeelezea masikitiko yake kutokana na kifo hicho ni kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Chanzo: mwananchi.co.tz