Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Iran na Kenya zaazimia kuimarisha ushirikiano sekta mbali mbali

Iran Keny SEKTA Iran na Kenya zaazimia kuimarisha ushirikiano sekta mbali mbali

Wed, 12 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Marais William Ruto wa Kenya na Ebrahim Raisi wa Iran wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika sekta mbali mbali. Hayo yamebainika katika hotuba za marais hao leo mjini Nairobi baada ya mazungumzo.

Rais wa Iran aliwasili mjini Nairobi alfajiri ya leo kikiwa ni kituo cha kwanza cha safari yake ya kuzitembelea nchi tatu za Afrika za Kenya, Uganda na Zimbabwe.

Akizungumza mjini Nairobi, Raisi amesema Iran na Kenya zina uwezo mkubwa wa kuimarisha ushirikiano na kuongeza kuwa, kumewekwa lengo la kuimarisha kiwango cha mabadilishano ya kiuchumi mara 10 zaidi ya ilivyo sasa.

Katika hotuba hiyo baada ya Kenya na Iran kutiliana saini mapatano matano katika nyanja mbali mbali, Raisi amesema uhusiano wa Iran na Kenya unezidi kuimarika. Aidha amesema, kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu na miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran imeweza kusimama kidete kukabiliana na vikwazo na sasa imepiga hatua katika sekta mbali mbali za kisayansi, kiteknolojia na kiuchumi.

Rais wa Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran ameshukuru serikali na watu wa Kenya kwa kumkaribisha na ameelezea matumaini kuwa, uhusiano wa Nairobi na Tehran utazidi kuimarika.

Rais Raisi amesifu sera ya Kenya ya kuweka mazingira rafiki kwa biashara za kigeni. Amesema makampuni zaidi ya Iran yataanzisha shughuli zake nchini Kenya na hivyo kufungua njia yao ya kufikia masoko mengine ya Afrika yenye zaidi ya watu bilioni 1.4.

Kwa upande wake, Rais Ruto amesema Kenya itatumia uhusiano mkubwa ilionao na Iran kupanua biashara. Ameongeza kuwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili bado kiko chini lakini kuna uwezekano wa kukua. Ameeleza kuwa Kenya na Iran zitaweka utaratibu utakaowezesha mauzo ya nje ya chai, kahawa na nyama zaidi.

Rais Ruto amesema kwamba Kenya pia itatumia uwezo wa Iran katika teknolojia na uvumbuzi ili kujiimarisha kimaendeleo.

Amedokeza kwamba kuanzishwa kwa Jumba la Ubunifu na Teknolojia la Iran mjini Nairobi ni jukwaa mwafaka kwa biashara za Iran na Kenya.

Marais Ruto na Raisi mapema leo walishuhudia kutiwa saini makubaliano mapya katika nyanja za kilimo, mifugo, utamaduni na turathi, habari, TEHAMA, uvuvi, makazi na maendeleo ya miji.

Kabla ya kuhutubia waandishi habari na mazungumzo ya jumbe za pande mbili, marais wa Iran na Kenya walikuwa na kikao cha faragha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live