Baada ya raia wa India waliopo Sudan kutoa wito kwa serikali yao kuwasaidia kuondoka nchini humo katika siku kadhaa zilizopita, hatimaye New Delhi Jumatatu imeanza operesheni inayoitwa Operation Kaveri, ya kuwaondoa raia wake waliokwama katika mzozo uliolikumba taifa hilo Afrika.
Waziri wa mambo ya nje wa India S. Jaishankar alisema India imeanza mchakato wa kuwaondoa raia wake kutoka Sudan. Jumatatu waziri huyo alitweet kwamba “Operation Kaveri” inaendelea kuwarejesha raia wetu nyumbani waliokwama nchini Sudan.”
Takriban raia 500 wa India Jumatatu walikuwa wamefika Port Sudan huku wengine engine wakiwa njiani. “Meli zetu na ndege ziko tayari kuwarejesha nyumbani. Tuna nia ya dhati ya kuwasaidia ndugu zetu nchini Sudan,” alisema Waziri.
Mapigano yalizuka nchini Sudan Aprili 15, kufuatia mivutano ya madaraka kati ya majenerali wawili wa juu nchini humo - mkuu wa jeshi na mtawala wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah Burhan, na kamanda wa kikosi chenye silaha kinachofadhiliwa na serikai cha Rapid Support Forces, RSF Jenerali Mohammed Dagalo.
Ndege za kivita zimeripotiwa kupiga mabomu kwenye maeneo ya RSF ambako pia ni makazi yenye watu wengi maeneo ya mjini, na pande zote mbili zilipambana mitaani kwa kutumia bunduki na makombora, huku ghasia zikiendelea kusambaa.
Maelfu ya watu wamejikuta wakiwa na uhaba mkubwa maji, chakula na dawa, wakilazimika kutoroka makwao, kulingana na shirika la afya duniani WHO. Zaidi ya watu 400 wameuwawa huku maelfu wakijeruhiwa ndani ya siku 9 zilizopita tangu kuzuka kwa ghasia hizo.