Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Igad kusaka suluhu mzozo Ethiopia, Somalia

IGAD IGADDD.png Igad kusaka suluhu mzozo Ethiopia, Somalia

Mon, 15 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakuu wa nchi za umoja wa IGAD, wanatarajiwa kukutana Alhamisi, Januari 18, 2024 nchini Uganda kujadili mizozo ya kidiplomasia inayoendelea kati ya nchi za pembe ya Afrika ikiwemo mvutano kati ya Somali na Ethiopia iliyoingia kwenye makubaliano ya kijeshi na matumizi ya bahari ya Somaliland.

Mvutano huo ulioshika kasi hivi sasa, huku Somalia ikisema mkataba ulioingiwa kati ya Ethiopia na jimbo lililojitenga la Somaliland, unaingilia uhuru wake.

Mkataba huo unairuhusu Ethiopia kutumia baharí ya Shamu na kujenga kambi yake ya kijeshi katika jimbo la Somaliland ambalo lilitangaza kujitenga na Somalia tangu miaka ya 1990 lakini Somalia imekuwa ikikana uhuru wa jimbo hilo.

Hali hiyo imeendelea kuzua hofu na wasiwasi kati ya Ethiopia na Somalia huku Rais wa Somali, Hassan Sheikh Mohammud akiifananisha Serikali ya Ethiopia kama kundi la Al Shabab na kuelezea kitendo chake kama cha kigaidi.

Taarifa ya mkutano huo imetolewa na Rais wa Djibouti, Ismail Omar Guelleh, ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa muungano wa Igad kupitia barua kwa nchi wanachama wa umoja huo.

Mkutano huo unakwenda kufanyika kufuatia Somalia kuendeleza msimamo wake kwamba jimbo hilo bado halijajitenga na mkataba ulioingia na Ethiopia haiutambui zaidi ya kuingilia sehemu ya nchi yake.

Kwa mujibu wa Kituo cha RFI Swahili kupitia taarifa yake imemnukuu Mkuu wa masuala ya diplomasia ya Somaliand, Essa Kayd, ameitaka Serikali ya Addis Ababa kulitambua jimbo hilo kama nchi huru, ili kutekeleza makubaliano yaliyoafikiwa.

Licha ya Somaliland kujitangazia uhuru wake, haitambuliwi na jumuiya ya kimataifa, inayohofia kuwa, iwapo jimbo hilo litakuwa huru, maeneo mengine kwenye pembe ya Afrika yatataka kujitawala na hivyo kutikisa ukanda huo.

Mzozo mwingine utakao jadiliwa

Mazungumzo hayo pia yatagusia suala la mzozo unaoendelea nchini Sudan inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mzozo wa madaraka kati ya jeshi la Serikali na wapiganaji wa RSF kuanza mapigano mwezi Aprili mwaka jana.

Igad imekuwa ikiongoza juhudi za kikanda ili kusuluhisha usitishaji mapigano kati ya pande zinazozana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live