Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kithure Kindiki amesema vifo vya watu wa madhehebu ya Shakahola ni uhalifu 'uliopangwa ukapangika'.
Waziri huyo alisema hayo leo Jumanne baada ya kuwasili mjini Malindi kusimamia zoezi la ufukuaji wa makaburi, ambao ulisitishwa wiki iliyopita kwa sababu ya hali mbaya ya hewa.
"Nina wasiwasi huenda kuna makaburi mengi," Prof Kindiki alinukuliwa na chombo cha Nation na kuongeza kuwa ufukuaji wa makaburi unaweza kuchukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa hapo awali.
"Madhara mi makubwa sana, makaburi 20 ya watu wengi yanafukuliwa kwa sasa. Hii sio mwisho," alisema.
Alipozungumza na wanahabari, Prof Kindiki pia aliweka wazi kuwa maafisa wa upelelezi wanawafuatilia walioshirikiana na kiongozi wa madhehebu ya Kilifi Paul Mackenzie.
Kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki mwezi uliopita kumeishangaza nchi hiyo katika kile kilichopewa jina la "mauaji ya halaiki ya msitu wa Shakahola".
Zaidi ya watu 100 wameripotiwa kufariki kwa ibada ya kufunga mpaka kufa inayodaiwa kuhimizwa kwa waumini kupitia viongozi wao.