Kundi la Islamic State (IS) limesema limewaua Wakristo wanne, akiwemo mtawa wa Kiitaliano, katika shambulio lililotokea katika jimbo la Nampula kaskazini mwa Msumbiji siku ya Jumanne.
Ilitoa dai hilo siku iliyofuata kupitia akaunti zake kwenye programu ya kutuma ujumbe ya Telegram, kwa jina la kinachojulikana kama tawi la Mkoa wa Msumbiji.
Vyombo vya habari vya kawaida viliripoti Jumatano kwamba mtawa wa Kiitaliano mwenye umri wa miaka 83, aliyetambulika kama Sista Maria De Coppi, aliuawa kwa kupigwa risasi na wanamgambo waliovamia kijiji cha Chipene wilayani Memba ambako mmishonari wa Kikristo anaishi.
Watu kadhaa waliripotiwa kukatwa vichwa katika shambulio hilo.
Katika madai yake, IS ilisema ilimuua mtawa huyo kwa sababu ‘’alijishughulisha kupita kiasi katika kueneza Ukristo’’.
Pia ilijigamba kuwa wanamgambo wake walichoma kanisa, magari mawili na ‘’mali zingine za mmisionari katika eneo hilo’’, kabla ya kudaiwa kurejea salama katika nyadhifa zao.
Kabla ya shambulio hili, IS ilikuwa imedai kutekeleza shambulio la kwanza na la pekee huko Nampula mnamo Juni wakati pia ilidai kuvamia kijiji cha Memba na kudaiwa kumkata kichwa Mkristo mmoja.
Nampula iko kusini mwa mkoa wa Cabo Delgado ambapo shughuli za IS zimejikita.
Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amethibitisha kutokea kwa shambulizi la hivi punde mjini Nampula.