Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) ambayo ni taasisi ya Umoja wa Mataifa inayojihusisha na uhamiaji pamoja na washirika 27 wengine wametoa mwito wa kutengwa dola milioni 112 za Kimarekani kwa ajili ya kutoa msaada wa haraka kwa zaidi ya wahamiaji milioni 1.4 walioko kwenye eneo la Pembe ya Afrika, Yemen na kusini mwa Afrika.
Katika taarifa yake ya jana Ijumaa, IOM imesema kuwa, fedha hizo zitatumika kutoa msaada wa kibinadamu na masuala ya maendeleo kwa ajili ya wahamiaji wanaoondoka nyumbani kutafuta nafasi bora za kazi, na wakati mwingine kuepuka migogoro, ukosefu wa usalama na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa.
Sehemu moja ya taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya imesema: "Miaka iliyopita imetuonyesha mafanikio makubwa tunayoweza kupata wakati tunapofanya kazi pamoja." Majanga ya kimaumbile kama ukame ni miongoni mwa sababu za watu kuhatarisha maisha yao na kuingia kwenye uhamiaji haramu
Kwa mujibu wa Rana Jaber, mkurugenzi wa IOM kanda ya Mashariki na Pembe ya Afrika, njia ya mashariki kutoka Pembe ya Afrika hadi Yemeni na Mataifa ya Ghuba ya Uajemi, pamoja na njia ya kusini kutoka Pembe ya Afrika kupitia Kenya na Tanzania hadi kusini mwa Afrika, ni kati ya maeneo hatari sana kwa wahamaji duniani.
Amesema: "Tuna imani kwamba tunaweza kupata mafanikio makubwa zaidi mwaka huu wa 2024 na tunaweza kuendelea kuokoa maisha na kutoa ulinzi na kupata suluhisho endelevu."
Katika safari zao, wahamiaji wengi hukumbwa na hatari za kutishia maisha ikiwa ni pamoja na njaa, hatari za kiafya na kutumbukia mikononi mwa magenge hatari ya magendo haramu ya binadamu na wahalifu wengine. Shirika la uhamiaji la IOM linasema mara nyingi wahamiaji hao huwa wanahitaji mno matibabu, chakula, maji, malazi na misaada ya kisaikolojia na kijamii.