Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) wa Kenya, Japhet Koome ametoa ufafanuzi kuhusu taarifa zilizombazwa mitandaoni kuwa Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta amepunguziwa ulinzi.
Taarifa hizi ziliibua sintofahamu kutokana na kuwepo mvutano wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta anayeunga mkono upande wa upinzani unaoongozwa na Raila Odinga.
Akizungumza leo jijini Mombasa, IGP Koome amesema kuwa wamepunguza idadi ya walinzi binafsi wa rais mstaafu kwa mujibu wa sheria, na kwamba haina maana kuwa wamepunguza ulinzi anaostahili.
Ameeleza kuwa msafara wa Rais aliye madarakani uko chini ya Msaidizi wa IGP, lakini anapostaafu yanafanyika mabadiliko ambapo msafara wake unakuwa chini ya kiongozi wa polisi anayeripoti kwa Msaidizi wa IGP.
Alisisitiza kuwa utaratibu huo ulikuwepo kwa mujibu wa sheria tangu enzi za rais wa zamani, Arap Moi.
“Kwahiyo, kwa lolote linalofanyika kwa nia njema IGP yupo. Kama kuna kiongozi yeyote ana shida anaweza kumfikia. Kazi yetu ni kuhakikisha kuwa tunatenda haki na kutimiza wajibu wa kumlinda kila kiongozi wa taifa hili bila upendeleo,” alisema IGP Koome.
Kiongozi huyo wa polisi aliongeza kuwa hata ulinzi wa wake wa wastaafu umebadilika kulingana na maelezo aliyoyatoa.
Wiki hii, kulikuwa na mvutano wa kurushiana maneno kati ya Rais Ruto na Kenyatta. Ruto alimshtumu Kenyatta kwa kufadhili mikutano na maandamano yanayopangwa na kambi ya Raila Odinga ili asilipe kodi katika biashara zake, lakini Kenyatta alikanusha taarifa hizo akidai ni maneno ya walioshindwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.