Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ICC yaamuru kulipwa fidia waathiriwa wa LRA Uganda

HUKUMU ICC yaamuru kulipwa fidia waathiriwa wa LRA Uganda

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) jana Jumatano walitoa amri ya kutolewa fidia ya zaidi ya euro milioni 52 (dola milioni 56) kwa maelfu ya waathiriwa wa ukatili wa kamanda aliyepatikana na hatia wa kundi la waasi wa Uganda la Lord's Resistance Army, Dominic Ongwen.

Dominic Ongwen alipatikana na hatia ya uhalifu 61 wa kivita na dhidi ya ubinadamu katika uamuzi uliotolewa na mahakama ya ICC mnamo Februari 2021.

Karibu waathiriwa 50,000 watakaofaidika na agizo hilo ni pamoja na watoto waliokuwa wanajeshi na watoto waliozaliwa kutokana na ubakaji wa wapiganaji wa kundi la Lord's Resistance Army (LRA) na mimba za kulazimishwa.

Hata hivyo majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wamesema Ongwen, mwanajeshi wa zamani ambaye alipanda vyeo na kuwa mmoja wa makamanda wakuu wa waasi maarufu wa Lord's Resistance Army (LRA), hana rasilimali za kulipa fidia hiyo yeye mwenyewe. Hivyo wameiomba mahakama hiyo kulipa fidia hiyo kutoka kwenye mfuko wake wa Trust Fund for Victims.

Fidia hiyo itakuwa katika mfumo wa malipo ya mtu binafsi ya euro 750 kwa kila mwathiriwa na fidia za ziada za pamoja kama vile programu za ukarabati na vituo vya kumbukumbu.

Kamanda wa zamani wa kundi la waasi la LRA, Dominic Ongwen alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 25 jela mwaka 2021 kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, yakiwemo ya ubakaji, mauaji na utekaji nyara wa watoto. Kwa sasa anatumikia kifungo chake nchini Norway. Dominic Ongwen

Wakiongozwa na mbabe wa kivita aliyeko mafichoni Joseph Kony, waasi wa LRA waliwatia hofu Waganda kwa takriban miaka 20 wakipigana na serikali ya Rais Yoweri Museveni kutoka kambi za kaskazini mwa Uganda na nchi jirani. Wanamgambo hao wameangamizwa kwa kiasi kikubwa, lakini Kony anasalia kuwa mmoja wa watoro wanaosakwa sana na mahakama ya ICC.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live