Uganda imetangaza kwamba itaanza ujenzi wa kituo cha kwanza cha nyuklia nchini humo, Kiwanda cha Nyuklia cha Buyende, kwa ushirikiano na Shirika la Kitaifa la Nyuklia la China ambacho kitasaidia nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika kuendeleza uwezo wa matumizi ya amani ya nishati ya atomiki.
Hivi sasa barani Afrika, ni Afrika Kusini pekee iliyo na kiwanda cha kuzalisha umeme wa nyuklia, huku shirika la nishati la serikali la Russia, Rosatom, likiwa linaendelea na ujenzi wa kituo cha kwanza cha nyuklia cha Misri ambao ulianza mwaka jana.
Serikali ya Uganda imesema inachukua hatua madhubuti za kuunganisha nishati ya nyuklia katika uzalishaji wa umeme ili kuhakikisha usalama wa nishati na kutoa umeme wa kutosha kwa maendeleo ya viwanda.
Waziri wa Nishati na Madini Ruth Nankabirwa Ssenamu alisema katika taarifa yake kwamba: "Maandalizi ya kutathmini eneo la Kiwanda cha Umeme cha Nyuklia cha Buyende yanaendelea ili kuweka njia kwa mradi wa kwanza wa nishati ya nyuklia unaotarajiwa kuzalisha MW 2,000, huku MW 1,000 wa kwanza kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo 2031.”
Aliongeza kuwa kiwanda hicho kitajengwa takriban kilomita 150 kaskazini mwa mji mkuu Kampala, kama sehemu ya juhudi za kuongeza vyanzo vya umeme nchini na kuharakisha mchakato wa kupata nishati, safi ambayo ni sehemu muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Rais Yoweri Museveni alisema nchi hiyo ina hazina kubwa ya madini ya urani ambayo ingependa kunufaika nayo. Alisisitiza kuwa utawala wake una na hamu ya kutumia urani hiyo kujenga kinu cha kwanza cha nyuklia Afrika Mashariki.