Mshawishi maarufu wa Instagram kutoka Nigeria amefungwa kwa zaidi ya miaka 11 nchini Marekani kwa jukumu lake katika harambee ya kimataifa ya utapeli.
Hushpuppi, ambaye jina lake halisi ni Ramon Abbas, alidhihirisha maisha yake ya kitajiri kwenye ukurasa wake ambao ulikuwa na wafuasi milioni 2.8 hadi ulipolemazwa.
Jaji wa Los Angeles pia aliamuru alipe dola 1,732,841 ili kuwafidia waathiriwa wawili wa ulaghai.
Abbas atatumikia kifungo chake cha miezi 135 katika jela ya Marekani.
Mwaka jana alikiri makosa ya utakatishaji fedha.
Abbas alikiri kujaribu kuiba zaidi ya dola milioni 1.1 kutoka kwa mtu ambaye alitaka kufadhili shule mpya ya watoto nchini Qatar, nyaraka za mahakama huko California zilisema.
Tapeli huyo alimhadaa mwathiriwa wake kutoa fedha kwa ajili ya shule "kwa kutekeleza majukumu ya maafisa wa benki na kuunda tovuti ya uwongo", kulingana na taarifa kutoka kwa aliyekuwa Kaimu Mwanasheria wa Marekani Tracy Wilkinson kwenye tovuti ya idara ya sheria ya Marekani.
Washukiwa wengine pia walidaiwa kuhusika, idara ya sheria ya Marekani ilisema, huku Abbas akichukua jukumu muhimu.
Abbas pia alikiri "mipango mingine mingi ya mtandao na barua pepe ya maelewano ya barua pepe ambayo kwa jumla ilisababisha hasara ya zaidi ya dola milioni 24", idara ya sheria ya Marekani ilisema.
"Ramon Abbas... aliwalenga wahasiriwa wa Marekani na kimataifa, na kuwa mmoja wa wabadhirifu wa fedha zaidi duniani," Don Alway, mkurugenzi msaidizi anayesimamia Ofisi ya FBI ya Los Angeles, katika hati ya mahakama siku ya Jumatatu.