Benki ya Biashara ya Ethiopia imesema imerejesha huduma za kifedha katika baadhi ya miji kwenye jimbo lililokumbwa na vita la Tigray la kaskazini mwa nchi hiyo na kuwawezesha wakazi wa jimbo hilo kupata fedha zao baada ya kufungwa huduma hizo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Tangazo hilo lililotolewa jana Jumatatu ni matunda ya makubaliano ya amani kati ya serikali ya shirikisho na waasi wa Tigray yaliyotiwa saini mwezi uliopita nchini Afrika Kusini kwa shabaha ya kumaliza mzozo na vita vya umwagaji wa damu vilivyodumu kwa muda wa miaka miwili na kusababisha maafa makubwa ya kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia.
Katika taarifa yake, benki hiyo kubwa zaidi ya Ethiopia imesema: "Kufuatia makubaliano ya amani yaliyofikiwa hivi majuzi, matawi ya (CBE) tuliyo nayo katika miji ya Shire, Alamata na Korem yameanza kupokea pesa zinazotumwa kutoka nje na ndani ya nchi pamoja na kuweka pesa. Benki yetu ililazimika kusitisha huduma zake kwa sababu ya kukosekana usalama na utulivu katika sehemu ya kaskazini mwa nchi."
Jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia limekuwa chini ya mashinikizo makubwa yakiwemo ya kukatika mawasiliano kwa zaidi ya mwaka mmoja, na hivyo kufanya kuwa vigumu kwa waandishi wa habari kuripoti hali halisi ya watu maskini wa mashinani wa eneo hilo.
Tangu yalipotiwa saini makubaliano ya amani tarehe pili mwezi uliopita wa Novemba nchini Afrika Kusini, mapigano kati ya wanajeshi wa serikali ya shirikisho na waasi wa Tigray People's Liberation Front yamesimama huku waasi hao wakisema kuwa wameondoa asilimia 65 ya wanajeshi wake katika maeneo ya vita.
Misaada ya kibinadamu imekukwa ikiingia huko kaskazini mwa Ethiopia tangu makubaliano hayo yalipofikiwa, lakini bado kuna upungufu wa kuwafikia mahitaji yao idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo.