Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Historia nyingine Tanzania, Uganda

7e642d1f05fad4419da6be53fe6be931 Historia nyingine Tanzania, Uganda

Mon, 12 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

RAIS Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, wameshuhudia na kusaini mikataba inayoashiria kuanza kwa hatua kubwa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la kutoka Hoima Uganda kwenda Tanga nchini Tanzania.

Katika hafla hiyo iliypofanyika Ikulu ya Entebbe, Uganda, marais hao waliahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa na kufikia lengo la kukuza uchumi wa nchi hizo na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa jumla.

Samia na Museveni walishuhudia utiaji saini wa mkataba wa kwanza ambao ni wa uenyeji wa mradi kati ya Serikali ya Uganda na wawekezaji (Total na CNOCC), mkataba wa pili wa ubia ambapo Serikali za Tanzania na Uganda zimetiliana saini na kampuni hizo (Total na CNOCC) na mkataba wa tatu wa masuala ya kikodi na usafirishaji ambapo Serikali ya Uganda imetiliana saini na kampuni hizo (Total na CNOCC).

Pia, marais hao walitia saini tamko la pamoja kuhusu utekelezaji wa mradi huo na wameagiza vipengele vilivyobaki katika utekelezaji wa mradi huo vikamilishwe haraka.

Mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba la mafuta lenye kutumia teknolojia ya joto lenye urefu wa kilometa 1,445 ambapo kati yake kilometa 1,115 zinapita Tanzania.

Uwekezaji katika mradi huuo utarajiwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 3.5, utazalishaji ajira takribani 10,000 wakati wa ujenzi na utasafirisha mapipa bilioni 6.5 ya mafuta yaliyogundulika katika bonde la Ziwa Albert nchini Uganda kwenda Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alisema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni hatua muhimu si tu kwa Tanzania na Uganda, bali pia kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Wote tunafahamu kuwa mradi huu utakuwa na athari chanya katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi na una nguvu ya kimkakati,” alisema Samia.

Alitaja mafanikio mengine ya mradi huo kuwa ni pamoja na kuongeza mapato ya taifa, kuzalisha ajira, kukuza utangamano na kuinua ustawi wa jamii.

“Inatarajiwa kuwa zaidi ya fursa 10,000 za ajira zitazalishwa katika kipindi chote cha utekelezwaji wa mradi huo na hata baada ya kukamilika,” alisema.

Alisema pamoja na mafanikio ya kijamii, mradi huo pia utachochea biashara, uwekezaji na kufungua uwezo wa Afrika Mashariki katika eneo la mafuta na hivyo kukaribisha zaidi uwekezaji.

“Jambo la muhimu zaidi mradi huo utaongeza nguvu na ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi zetu mbili (Uganda na Tanzania) na kuongeza ushirikiano baina ya nchi na muingiliano wa watu.

Ninaamini kuwa mradi huu utakapokamilika utakuwa na faida kwa wote nchi zetu na jumuiya yetu kwa jumla,” alisema Rais Samia.

Alizipongeza pande zote mbili za Tanzania na Uganda na wadau wanaoshiriki katika ujenzi wa mradi huo kwa kujitolea kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kikamilifu huku akisisitiza masuala yaliyobaki ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi kujadiliwa na kukamilika.

“Ninaziomba pande zote kuendelea kufanyakazi kwa pamoja kupatiwa ufumbuzi kwa mambo yaliyobakia kuhakikisha mradi huu unatekelezwa vyema,” alisema.

Rais Samia alitoa mwito kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza jitihada za kuimarisha miundombinu ya barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege ili kuunga mkono uwekezaji huo pamoja na uwekezaji mwingine unaolenga kuimarisha uchumi na kuboresha maisha ya watu.

“Nchi zetu zina rasilimali za kutosha ikiwemo gesi, mafuta na madini ili kutumia vyema rasimali hizi kuna haja ya kuwa na miundombinu ya kisasa kwani bila hatua hiyo maendeleo ya kiuchumi itakuwa vigumu kuyafikia,” alisema

. Akaongeza: “Nina furaha kuwa nchi zetu sasa zinajenga miundombinu ya kimkakati ambapo pamoja na bomba hili, sasa nchi hizi zimejikita katika kujenga barabara za kisasa, viwanja vya ndege na miradi mikubwa ya kuzalisha umeme ikiwemo bomba hili.”

“Nahamasisha nchi zote kuendelea kujenga hii moiundombinu itakayojenga uchumi wetu.” Alisema ziara hiyo nchini Uganda ni ya kwanza kwake tangu aape kuwa Rais wa Tanzania kutokana na kifo cha Dk John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam.

Pamoja na hayo, Rais Samia alimhakikishia Rais Museveni kuwa serikali anayoiongoza itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano na uhusiano wake na Uganda ikiwa ni pamoja na kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano.

Awali, Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani alieleza hatua ya majadiliano kuhusu mradi huo kwa upande wa Tanzania ilipofikia na kubainisha kuwa, jumla ya mambo 56 yalijadiliwa na kufikiwa mwafaka.

“Tunawahakikishia kuwa utekelezaji wa mradi huu tutausimamia kwa kasi na ubunifu na weledi mkubwa ili ukamilike ndan ya miaka mitatu kama ilivyokubaliwa,” alisisitiza Kalemani

Chanzo: www.habarileo.co.tz