MADRID, HISPANIA. Mchezaji nyota wa Real Madrid, Eden Hazard atakosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Manchester City na ule wa El Clasico (dhidi ya Barcelona) baada ya kuvunjika mguu juzi kwenye mechi ambayo timu yake ililala kwa Levante kwenye La Liga.
Mbali ya kuikosa Manchester City katika mechi muhimu ya mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, ataikosa nyingine ya El Clasico dhidi ya mahasimu wao Barcelona, wikiendi ijayo.
Hazard aliyenaswa kwa Pauni 150 milioni za Uingereza kutoka Chelsea mwaka jana, alitoka uwanjani baada ya kuumia huku timu yake ikikumbana na kichapo cha bao 1-0.
Kuumia kwake kunamfanya awe nje ya uwanja kwa muda wote wa msimu uliobaki. Amevunjika mguu ikiwa ndio kwanza amerejea kuitumikia Los Blancos akitokea kwenye majeruha na hilo linaendeleza majanga kwenye msimu wake wa kwanza Bernabeu.
Staa huyo wa Ubelgiji amefunga bao moja tu msimu huu na kufanya uhamisho wake wa fedha nyingi kuonekana kuwa ni hasara tu. Hazard alikuwa nje ya uwanja kuanzia Novemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu ambapo alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya enka na katika kipindi hicho, amekosa mechi 20.
Wakati akitolewa uwanjani juzi kwenye dakika 67, ubao wa matokeo ulikuwa unasomeka 0-0.
Pia Soma
- Metacha aibeba Yanga ikilazimisha suluhu kwa Coastal Union Uwanja Mkwakwani
- Rapa Cardi B kuongoza tamasha la Unlocks Johannesburg
- Tyson Fury amkalisha Wilder raundi ya saba
Kipigo hicho kilikuwa cha kwanza kwa Real Madrid kwenye ligi tangu Oktoba ilipochapwa na Mallorca, mechi ambayo pia Hazard hakuwapo uwanjani.