Kinyang'anyiro cha kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Kenya unaotarajiwa Agosti 9, mwaka huu, kilivutia takriban wawaniaji hamsini.
Lakini ilipowadia muda wa wagombea hao kuwasilisha maombi yao kwa Tume huru ya uchaguzi IEBC ili kuona iwapo wametimiza yote yalioanishwa kuchambua nani ni Mtia nia na nani anastahili kuwa mgombea urais, orodha hiyo ndefu ilisalia na majina manne tu!
Nao ni mgombea wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, anayewania urais kwa mara ya tano tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini Kenya., naibu rais William Ruto anayewania kupitia tiketi ya chama cha UDA.
Wengine ni George Wajackoyah ,aliyezua mjadala katika mitandao ya kijamii kutokana na azma yake ya kutaka bangi ihalalishwe na mwisho David Mwaure wa chama cha Agano. Wafahamu viongozi hao kwa ufupi.
Raila Odinga: Bwana Odinga anaonekana kuwa mrithi wa kisiasa wa baba yake, Jaramogi Odinga. Alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa Kenya baada ya uhuru, lakini aliondoka serikalini mwaka wa 1966 baada ya kutofautiana na kiongozi wa wakati huo, Jomo Kenyatta, baba yake na rais wa sasa, Uhuru Kenyatta.
Jaramogi Odinga aliunga mkono ushirika na uhusiano wa karibu na nchi za Umoja wa Kisovieti na China, huku Jomo Kenyatta akiunga mkono ushirika wa Marekani na mataifa mengine yenye nguvu ya Magharibi.
Tofauti zao zilizidi kuwa mbaya, ambapo Jaramogi Odinga alifungwa kwa miezi 18 hadi alipoachiliwa huru mnamo mwaka 1971. Raila Odinga pia ni mfungwa wa zamani wa kisiasa, na anashikilia rekodi ya kuwa mfungwa wa kisiasa aliyetumikia kifungo cha muda mrefu zaidi nchini Kenya.
Mapambano yake dhidi ya udikteta wa chama kimoja yalimfanya awekwe kizuizini mara mbili (kutoka 1982 hadi 1988 na 1989 hadi 1991) wakati wa utawala wa mrithi wa Jomo Kenyatta na Daniel Arap Moi.
Hapo awali alifungwa kwa kujaribu kufanya mapinduzi mwaka wa 1982. Mpinzani wake wa karibu ni William Ruto, wa Chama cha United Democratic Alliance UDA Naibu wa sasa wa Rais anayejinadi kwa misingi ya kutetea maslahi ya wananchi wa tabaka la chini waliobandikwa jina 'Hustler'.
William Ruto: Maisha ya utotoni ya William Ruto ni mfano halisi wa maisha ya watoto wengi masikini Wakenya.
Alikwenda shule miguu peku, ambapo alivaa kwa mara ya kwanza viatu akiwa na umri wa miaka 15. Aliuza kuku na karanga kando ya barabara katika maeneo ya kijijini kwao katika mkoa wa Bonde la ufa (Rift Valley).
Kwa hiyo sio jambo la kushangaza kwamba anajielezea kama kiongozi wa masikini wakati anapogombea kiti cha urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 9 Agosti.
Bw Ruto anawania kiti hicho chini ya Muungano unaofahamika kama Kenya Kwanza, akitoa ahadi ya kukuza uchumi. Wagombea hao wawili wakuu wamekuwa wakitawala siasa za Kenya katika nyadhifa mbali mbali kwa miongo kadhaa sasa, wakizoeleka machoni na masikioni mwa Wakenya.
Profesa Wajackoyah: Lakini ni kujitosa kwa Profesa George Luchiri Wajackoyah katika kinyanganyiro cha uchaguzi wa rais 2022 ambako kumezua gumzo kweli kweli miongoni mwa Wakenya ambapo limeibua shauku hasa miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii na vijana.
Hamu ya kutaka kumfahamu zaidi imeongezeka baada ya Tume ya uchaguzi kumuidhinisha kuwa mgombea rasmi wa urais katika uchaguzi unaokuja ndani ya miezi miwili.
Mgombea huyu alizaliwa magharibi mwa Kenya eneo la Matungu. Ana umri wa miaka 61. Alilelewa katika mazingira magumu baada ya wazazi wake kuachana akiwa na umri mdogo sana.
Kama wasemavyo Waswahili ukikosa ziwa la mama hata la mbwa huamwa, alipata wahisani waliomshika mkono na angalau kumsaidia kupata elimu, akitolewa mfano aliyekuwa waziri wa elimu marehemu Joseph Kamotho aliyeelezewa masaibu ya Wajackoyah na kumsaidia kulipa karo yake ya shule ya upili.
Baadaye alisomea sheria katika vyuo vikuu mbali mbali duniani, akisemekana kuwa na zaidi ya shahada kumi za uanasheria.
Profesa Wajackoyah ni Mwanasheria mwandamizi aliyefunza katika vyuo vikuu mbali mbali ndani na nje ya nchi, akijulikana pia katika ubobezi wake mkubwa katika sheria za wakimbizi na uhamiaji, akiwakilisha na kuwatetea baadhi ya wanasiasa wa upinzani katika kanda ya Afrika Mashariki waliolazimika kukimbia uhamishoni.
Profesa Wajackoyah ni muasisi wa Chama cha Roots kinachokusudia kuhalalalisha bangi na inadi pakubwa uzalishaji na matumizi ya mmea huo.
Ameahidi iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Kenya, atajenga fursa za kazi hasa kwa vijana kwa kuruhusu uuzaji wa bangi ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa zao hilo pia litasaidia kupunguza mzigo wa madeni ya Kenya kwani utazalisha mapato makubwa. Bangi imeharamishwa nchini Kenya kuambatana na sheria za sasa.
Aidha ameahidi akiwa Rais, Kenya itakuwa na Mawaziri wakuu wanane kuendesha Serikali yake, atasimamisha Katiba kwa miezi sita na siku rasmi za kufanya kazi zitakuwa Jumatatu hadi Alhamisi badala ya Jumatatu hadi Ijumma.
David Mwaure Waihiga: Mgombea mwingine katika uchaguzi wa Agosti 2022 ni David Mwaure Waihiga, kiongozi wa Chama cha Agano kilichoanzishwa miaka kumi na sita iliyopita. Ni mwanasheria mwandamizi mwenye tajriba ya kuwa wakili kwa miaka thelathini na tano na pia ni Mhubiri.
Hajaonekana sana hadharani akinadi sera zake lakini katika ruwaza yake amejikita zaidi katika ahadi kuwa akichaguliwa kuwa Mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta anayeondoka madarakani baada ya kukamilisha mihula miwili madarakani, atakabiliana vilivyo na ufisadi.
Kiongozi huyo anasema ufisadi ndiyo jinamizi kubwa linaloizonga Kenya na limetokana na kuwachagua viongozi wafisadi, wasio waadilifu wanaotuhumiwa katika kashfa mbali mbali za uporaji na ubadhirifu wa mali za umma.
Katika manifesto yake ameapa kuleta uongozi mpya Kenya utakaojikita katika misingi ya Usawa,uwazi,uadilifu, Umoja na haki. Bwana Waihiga anasema angependa kukumbukwa kama kiongozi aliyetokomeza ukabila,urasimu, usimamizi mbaya na kurejesha mali iliyofichwa na mafisadi nje ya nchi.
Bwana Waihiga awali mwaka 2011 alijaribu kuwania kiti cha eneo bunge la Kamukunji bila ya mafanikio. Mwaka 2013,aliwania ugavana wa Kaunti ya Lamu na Mnamo mwaka 2021, aliidhinishwa na Chama chake kuwania Ugavana wa Kaunti ya Nairobi kufuatia Gavana Mike Mbuvi kuondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye lakini hakukuwa na uchaguzi ulioendeshwa kujaza nafasi hiyo baada ya mahakama kutoa uamuzi naibu gavana Ann Kananu kushikilia ugavana wa Nairobi.
Bwana David Mwaure Mwaiga ana imani ana sifa zote za kustahili kuwa kiongozi ajaye wa Kenya. Lililosalia ni kujua mbivu na mbichi ifikapo Agosti 9,2022, miezi miwili kutoka sasa. Wapiga kura waamuzi wa nani kati ya wagombea wanne wa urais watampa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.