Rais William Ruto amewaonya maafisa wa polisi dhidi ya mauaji ya kiholela ya waandamanaji wanaoipinga serikali, huku - kwa upande mwingine - pia akisisitiza kwamba kila mtu lazima afuate sheria.
Akizungumza katika ziara yake katika Kaunti ya Murang'a siku ya Ijumaa, Rais amesisitiza kuwa kuwa serikali yake itakabiliana na wale wanaovunja sheria iwe katika maafisa wa usalama au umma kuhusiana na maandamano yanayoendelea kuongozwa na upinzani.
Alirejelea kuhusu ahadi aliyoitoa baada ya kula kiapo cha urais ambapo aliahidi kutokomeza utovu wa nidhamu na kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa na kuongeza kuwa ataleta utulivu nchini.
Mkuu huyo wa nchi aliongeza kuwa hakuna mtu atakayeruhusiwa kusababisha ghasia, fujo na uharibifu wa mali na kuondoka nazo.
“Hatutaruhusu kuvunja sheria na kuua watu kiholela. Vile vile tulivyosema tutaondoa mauaji ya kiholela ni sawa na jinsi tulivyojitolea kuhakikisha hakuna adhabu. Huwezi kuharibu mali, kusababisha ghasia na machafuko na [usiwajibike] ... hautaweza! Rais Ruto alionya.
“Tunaomba maafisa wetu wa kulinda sheria wawe waangalifu, wasimame na ninataka kupongeza vyombo vyetu vya usalama kwa kuwa na weledi wa jinsi ambavyo vimewashughulikia watu hawa. Wahalifu lazima washughulikiwe kwa uthabiti, na kuhakikisha kuwa kila mtu anaheshimu utawala wa sheria."
Akiwatetea maafisa wa usalama ambao wameshutumiwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, Bw Ruto alisema wanafanya tu kazi yao ya kuhakikisha kuna amani na utulivu.