Wakazi wa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, wanaripoti kuwa mji huo umeshuhudia hali ya utulivu kwa mara ya kwanza tangu mapigano yaanze katikati ya mwezi wa Aprili, huku usitishaji vita uliotangazwa tangu Jumatatu ukizingatiwa kwa kiasi kikubwa.
Dakika chache baada ya mapatano kuanza Jumatatu jioni, ndege za jeshi zilishambulia maeneo ya Vikosi maalum ya kijeshi, lakini hakukuwa na mashambulio ya anga katika mji mkuu baada ya hapo, kulingana na mkazi wa eneo hilo aliyezungumza na BBC.
Hata hivyo, milio ya risasi inasikika mara kwa mara huko Khartoum.
Kwa mujibu wa AFP, ikitoa mfano wa wakazi wa eneo hilo, miji ya El Geneina na Nyala katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan, ambako mapigano makali pia yalikuwa yakiendelea, sasa pia imekuwa kimya.
Mapigano yalizuka nchini Sudan tarehe 15 Aprili kufuatua mvutano wa madaraka kati ya majenerali wawili wenye ushawishi mkubwa nchini humo.
Mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, anapigana na naibu wake, kamanda wa Kikosi maalum, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemeti.
Marekani na Saudi Arabia wapatanishi kati ya pande zinazozana.
Chini ya shinikizo lao, makubaliano kadhaa tayari yametangazwa, na yote yalivunjika, lakini hii ya hivi karibuni, kulingana na Marekani, ni tofauti na ile ya awali, makubaliano ya kusitisha mapigano yamezingatiwa.