Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hasira za upinzani zatikisa Kenya na Afrika Kusini

Hasira Za Upinzani Zatikisa Kenya Na Afrika Kusini Hasira za upinzani zatikisa Kenya na Afrika Kusini

Mon, 20 Mar 2023 Chanzo: Bbc

Kenya na Afrika Kusini zipo katika hali ya wasiwasi leo Jumatatu kutokana na wito wa maandamano yaliyopangwa huku vyama vya upinzani katika nchi zote mbili vikiwataka watu wasifanye kazi.

Nchini Kenya, vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kwamba kumekuwa na msururu mkubwa wa maafisa wa usalama katika mji mkuu, Nairobi, siku ya Jumatatu hasa karibu na majengo muhimu ya serikali.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga anapanga maandamano nchi nzima dhidi ya Rais William Ruto na serikali yake.

Bw Odinga anasema kuwa maandamano hayo yatakuwa dhidi ya gharama ya juu ya maisha na kile anachokiita urais haramu.

Huku kukiwa na hofu ya kutokea vurugu, polisi wameonya kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa kwa yeyote atakayevuruga amani.

Rais William Ruto amesema haoni sababu ya maandamano hayo na amemshutumu Bw Odinga kwa kutishia nchi kwa ghasia na machafuko.

Bw Odinga anasema watakuwa na amani, ingawa kihistoria, ni kinyume chake wakati maandamano yanapofanywa.

Kwa upande mwingine nchini Afrika Kusini, wanajeshi elfu kadhaa wanatumwa kote nchini kusaidia kulinda miundombinu muhimu wakati wa maandamano hayo.

Chama cha upinzani chenye itikadi kali, Economic Freedom Fighters, kimetoa wito kwa watu kutofanya kazi na kusaidia kusimamisha shughuli za nchi.

Inataka rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ajiuzulu kutokana na jinsi anavyoshughulikia uchumi.

Kuna mfadhaiko na hasira nyingi nchini Afrika Kusini kwa sababu ya hali ya uchumi, ukosefu wa ajira, ufisadi na kukatika kwa umeme bila kukoma.

Lakini bado haijabainika ni kiasi gani cha uungwaji mkono kitakuwa cha kusitishwa shughuli kwa taifa kulikoitishwa na chama chenye msimamo mkali cha Economic Freedom Fighters.

Chanzo: Bbc