"Hakuna mtu mwenye akili timamu anayeweza kukubaliana" kwamba Rais aliye madarakani Félix Tshisekedi alishinda kihalali muhula wa pili katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, mgombea wa upinzani amesema.
Katika mahojiano na kipindi cha Newsday cha BBC mnamo Jumanne, Martin Fayulu alitoa maoni mapya ya kufutwa kwa matokeo ya Jumapili.
Maafisa walisema Bw Tshisekedi alishinda karibu 73% ya kura.
Uchaguzi huo, ambao ulifanyika tarehe 20 Desemba, ulikumbwa na matatizo mengi ya vifaa na kiufundi.
Kufuatia kutangazwa kwa matokeo hayo, Bw Fayulu na wagombea wengine kadhaa wa upinzani walidai kuwa kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi na kukithiri kwa dosari.
Ujumbe wa uchunguzi unaoendeshwa na Kanisa Katoliki na makanisa ya Kiprotestanti pia ulibainisha "matukio mengi ya ukiukaji".
Akizungumza na BBC, Bw Fayulu alisema kuwa kutokana na umati wa watu waliokusanyika kwenye mikutano yake ya kampeni, wazo la kwamba alipata asilimia 5 pekee ya kura ni la kushangaza.
Aliongeza: "Tshisekedi hawezi kunishinda hata hivyo, hawezi kunishinda! "Watu wa Congo wako pamoja nami. Hakuna atakayemfuata Tshisekedi.
Anaweza kwenda kwa nguvu, lakini hakuna atakayemfuata." Bw Fayulu alitoa wito wa kufanyika uchaguzi mpya, matakwa ambayo yamekataliwa na msemaji wa serikali ya DR Congo na Waziri wa Habari Patrick Muyaya.
"Ni kweli kulikuwa na matukio lakini matukio haya hayakuweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa urais," Bw Muyaya alisema katika mahojiano ya awali na kipindi cha Newsday cha BBC.
"Ni sawa ikiwa wanataka kutumia njia za kisheria kuwania uchaguzi. Hiyo ni sheria. Wana haki ya kufanya hivyo lakini wakati huohuo wanapaswa kuhakikisha kwamba wanaweza kutoa uthibitisho wa kile wanachobishana,” Bw Muyaya aliongeza.
Alisema kuwa serikali "haitavumilia machafuko" kutoka kwa wanasiasa wa upinzani wasiofurahishwa na matokeo ya uchaguzi.