Kiongozi wa utawala wa zamani wa serikali wa kijeshi wa Guinea, Moussa Dadis Camara, ambaye jana asubuhi alitoroka kwenye gereza kuu la Conakry, mji mkuu wa Guinea, ametiwa mbaroni tena.
Hayo yametangazwa na Mkuu wa Jeshi la Guinea Ibrahima Sory Bangoura katika taarifa rasmi kwa vyombo vya habari na kuongeza kuwa, Moussa Dadis Camara yuko salama na hivi sasa amerudishwa katika gereza kuu la Conakry.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, maafisa wengine wawili wa kijeshi wa zamani waliiotoroka na Camara jana asubuhi ambao ni Kanali Moussa Tiegboro Camara na Kanali Blaise Gomou, nao pia wamekamatwa tena na kurudishwa jela.
Hata hivyo taarifa hiyo imesema kuwa, afisa mwingine wa serikali ya zamani ya Guinea Claude Pivi ambaye naye alitoroka gerezani jana pamoja na Camara, bado hajapatikana na msako unaendelea kuhakikisha na yeye anatiwa mbaroni na kurudisha jela.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Mahakama ya Rufaa ya Conakry ametoa maagizo ya kufunguliwa mashtaka mazito dhidi ya wafungwa wote wanne waliotoroka jela jana Jumamosi kwenye operesheni iliyofanyw ana makomandoo wenye silaha.