Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ghala la silaha lalipuka Chad, laua tisa na kujeruhi zaidi ya 40

Ghala La Silaha Ghala la silaha lalipuka Chad, laua tisa na kujeruhi zaidi ya 40

Thu, 20 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Milipuko mikubwa iliyosababishwa na moto imetokea katika ghala la silaha za kijeshi katika mji mkuu wa nchi hiyo, N’Djamena na kusababisha vifo vya watu tisa na wengine 46 kujeruhiwa.

Shirika la Habari la AFP limesema moto huo ulianza Jumanne jioni na kusababisha milipuko hadi usiku wa kuamka jana Jumatano ambayo imetikisa majengo hadi umbali wa kilomita saba huku miale ya moto ikionekana angani.

Waziri wa Afya, Abdelmadjid Abderahim amewaambia waandishi wa habari kuwa idadi ya vifo huenda ikaongezeka kwani wengi wa majeruhi hao, wako katika hali mbaya.

Msemaji wa Serikali ya nchi hiyo, Abderaman Koulamallah amesema sababu ya milipuko hiyo si uhalifu, hata hivyo uchunguzi unaendelea.

Amesema moto huo na milipuko imesababisha wakazi wa wilaya hiyo ya Goudji kushtuka kutoka usingizini.

Mashuhuda waliokuwepo katika eneo hilo wamesema anga liligeuka jekundu kutokana na milipuko na moto huku mitetemo mizito ikisikika.

Akizungumza eneo la tukio, Rais Mahamat Idriss Deby amesema hali imedhibitiwa na amewataka raia wa eneo hilo kuwa watulivu.

“Hii si mara ya kwanza kwa milipuko kama hiyo. Hii inapaswa kutufundisha somo ili kuanzia sasa tusije tukajenga tena maghala na maduka katikati ya jiji,” amesema Rais Deby.

Matukio ya moto na milipuko katika ghala za silaha, yamewahi kutokea maeneo mbalimbali hata Tanzania ambapo Aprili 29, 2009 mabomu yalilipuka katika kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) KJ 671 Mbagala na kusababisha vifo vya watu 25 huku mamia ya watu wakijeruhiwa na familia nyingi kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomoka na nyingine kupata nyufa.

Pia, watu 20 walifariki kutokana na milipuko katika kambi ya Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Alhamisi Februari 16, 2011.

Chanzo: Mwananchi