Mkuu wa benki kuu ya Ethiopia amebadilishwa huku nchi hiyo ikiendelea kukabiliwa na viwango vya juu vya mfumuko wa bei.
Yinager Dessie aliteuliwa kuwa gavana wa Benki ya Kitaifa ya Ethiopia (NBE) mnamo 2018 muda mfupi baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuingia madarakani.
Nafasi yake imechukuliwa na Mamo Mihretu, ambaye hapo awali alikuwa mshauri wa Waziri Mkuu wa masuala ya kiuchumi na baadaye akasimamia uwekezaji , taasisi ya fedha ya serikali na mashirika makubwa ya serikali kama Ethiopian Airlines na Ethio Telecom katika ofisi yake.
Gavana anayeondoka ameacha thamani ya sarafu ya nchi hiyo- birr ikiwa imeshuka dhidi ya dola na kukiwa na kiwango cha juu cha mfumuko wa bei.
Mfumuko wa bei wa mwaka hadi mwaka umebaki juu ya 20% tangu 2020, na kufikia zaidi ya 33% mwaka jana.
Bw Abiy pia ameteua mawaziri wanne wapya kuchukua nyadhifa zilizoachwa hivi karibuni zikiwemo za wizara za migodi na uchukuzi. Uteuzi wote unapaswa kuidhinishwa na baraza la chini la bunge.