Gavana wa Meru Kawira Mwangaza amekamatwa. Mwangaza alikamatwa alipokuwa akiendesha mpango wa Okolea katika eneo la Ruiga ya Kati huko Imenti.
Katika taarifa yake baada ya kukamatwa, Gavana Mwangaza alithibitisha kuwa kweli yuko mikononi mwa polisi.
Hata hivyo alilaumu mamlaka kwa kushindwa kuendelea na hatua zinazofuata za taratibu za kisheria baada ya kukamatwa kwake. Kulingana na Gavana, maafisa hao wa polisi 'wamemzuilia' kwenye gari la polisi.
"Niko chini ya ulinzi. Maafisa wa polisi hawataki kunipeleka Kituo ili kufungua mastaka. Wamenishikiliwa kwenye gari hili la polisi kwa saa mbili sasa," alisema.
"Inasikitisha kuona juhudi za kulemaza harakati za kuleta maendeleo ambazo zinakusudiwa kusaidia masikini katika jamii yetu vitisho kama hivyo visiruhusiwe kutatiza maendeleo katika jamii ya Wameru," aliongeza.
Gavana huyo alisema maafisa wa polisi walitumwa kutatiza utekelezaji wa mpango huo.Awali gavana huyo alikuwa ametangaza kwamba angesambaza ng'ombe kwa familia zenye mahitaji, chini ya mpango wa Okolea.