Mamlaka nchini Gabon imezima intaneti na kutangaza marufuku ya kutotoka nje usiku hadi asubuhi wakati upigaji kura ukimalizika nchini Jumamosi.
Waziri wa mawasiliano Rodrigue Mboumba Bissawou ametangaza hatua hizi kupitia televisheni ya taifa , akieleza kwamba zimenuiwa "kukabiliana na kusambaa kwa wito wa ghasia na taarifa za uongo". Hatua hiyo inafuata malalamiko ya upinzani kuhusu hitilafu zilizoshuhudiwa katika uchaguzi Jumamosi.
Mapema Jumamosi, mpinzani mkuu katika uchaguzi huo wa urais, Albert Ondo Ossa anadai kulaani alichokitaja kuwa “uongo uliopangwa.”
Msemaji wa muungano rasmi wa upinzani, Alternance 2023, amezitaja hatua hizo za serikali kuimarisha usalama kama hatua zilizovuka mpaka na kuongeza kwamba mamlaka hazitaki kuona maendeleo ya demokrasia nchi humo.
Raia wamepiga kura nchini kumchagua rais, wabunge na madiwani. Vituo kadhaa vya kupiga kura vilichelewa kufungiliwa.
Rais wa sasa Ali Bongo ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 14 anatafuta kuchaguliwa kuhudumu kwa muhula wa tatu.