Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Gabon yatangaza Baraza la Mawaziri

Gabon Gabobnn Gabon yatangaza Baraza la Mawaziri, mwanamke apewa wizara ya ulinzi

Mon, 11 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya mpito ya Gabon imetangaza Baraza jipya la Mawaziri, na kumteua mwanamke kuwa waziri wa ulinzi.

Hayo yanajiri wiki moja tu, baada ya Jenerali Brice Oligui Nguema, ambaye aliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyoung'oa madarakani utawala wa makumi ya miaka wa familia ya Bongo, kuapishwa Jumatatu iliyopita kuwa "rais wa serikali ya mpito" ya Gabon.

Taarifa zaidi zinasema, Jenerali Brigitte Onganoa ameteuliwa kuwa waziri wa ulinzi huku Luteni Kanali Ulrich Manfoumbi akipatiwa nafasi ya waziri wa mawasiliano na kubakia kuwa msemaji wa Kamati ya Mpito na Marejesho ya Taasisi (CTRI), muundo ulioundwa baada ya mapinduzi ya Agosti 30.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Waziri Mkuu wa mpito Raymond Ndong Sima ni kuwa, Regis Onanga Ndiaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni huku Mays Mouissim akiteuliwa kuwa waziri wa uchumi.

Baraza hilo la mawaziri linaundwa na mawaziri 26. Mawaziri watatu wa serikali iliyopinduliwa na Ali Bongo wamebakishwa katika nafasi zao.

Serikali ya kijeshi ya Gabon, ambayo ilinyakua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea wiki iliyopita, majuzi ilimteua kiongozi wa zamani wa upinzani, Raymond Ndong Sima, kuwa waziri mkuu wa serikali yake ya mpito.

Sima, ambaye ni mwanauchumi mwenye umri wa miaka 68, alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Ali Bongo, ambaye aliondolewa madarakani na maafisa wa kijeshi mnamo Agosti 30. Aliwahi kuwa waziri mkuu wa Bongo kuanzia mwaka 2012 hadi 2014, kisha akajiuzulu na kugombea urais dhidi yake mwaka 2016 na akawa tena sehemu ya muungano wa upinzani katika uchaguzi wa mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live