Kikosi tawala cha kijeshi nchini Guinea kimesema rais aliyeondolewa madarakani Alpha Condé amehamishwa na kupelekwa nyumbani kwa mkewe katika mji mkuu wa Conakry.
Kamati ya inayoongoza nchi hiyo (CNRD), ilisema katika taarifa iliyotangazwa kwenye televisheni ya serikali kwamba Bw Condé sasa yuko na mkewe, Hadja Djene Kaba Condé.
Ilisema "itaendelea kumpatia mkuu huyo wa zamani wa nchi heshima anayostahili bila shinikizo la kitaifa au kimataifa".
Rais aliyeondolewa madarakani mwenye umri wa miaka 83 alikuwa akishikiliwa kwa siri tangu alipoondolewa madarakani katika mapinduzi ya tarehe 5 Septemba.
Alikuwa ameiongoza Guinea tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2010, katika makabidhiano ya kwanza ya mamlaka ya kidemokrasia nchini Guinea.
Guinea ilisimamishwa kutoka muungano wa kanda ya Afrika Magharibi, Ecowas, kufuatia mapinduzi hayo.
Ecowas pia iliweka marufuku ya kusafiri na kufungia mali ya viongozi wa mapinduzi ya Guinea na familia zao huku ikitaka Bw Condé aachiliwe bila masharti.