Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fahamu kiiniu cha maandamano Kenya, mswada unaopingwa huu hapa

POLISI KENYA DG Fahamu kiiniu cha maandamano Kenya, mswada unaopingwa huu hapa

Tue, 25 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakenya wanaandamana kupinga mswada mpya wa sheria fedha unaotoa mapendekezo ya ushuru ambayo hayakubaliwa na wananchi wengi ambayo yameibua hasira kote nchini.

Mswada huo tata, ambao una vifungu vinavyoonekana kuwatwisha mzigo mkubwa raia wa kawaida na wafanyabiashara, umezua kilio kikubwa kutoka kwa wananchi ambao tayari wameelemewa na gharama ya juu za maisha.

Yameibuka maandamano yanayoongozwa na vijana, ambayo, ingawa kwa kiasi kikubwa yamekuwa ya amani, yamesababisha takriban kifo kimoja na mamia ya majeruhi pamoja na kukamatwa kwa mamia ya watu ambayo yote yamelaaniwa na wanasheria na makundi ya haki za binadamu.

Serikali imetupilia mbali baadhi ya mapendekezo yenye utata, lakini imechukua hatua chache kupunguza hasira za wananchi.

Wengi sasa wanataka muswada wote uondolewe ingawaje tayari wabunge wamepitisha baadhi ya marekebisho yaliyopendekezwa na serikali ili kutuliza hasira za umma.

Katika mitandao ya kijamii, kumekuwa na wito wa maandamano na madai kwamba wabunge wapinge nyongeza hiyo ya ushuru.

Ushuru wa bidhaa za msingi

Marekebisho ya mswada huo yanaonekana kupitishwa lakini baadhi ya vifungu vyenye utata vilivyowekwa hapo awali ni pamoja na mpango wa kuanzisha ushuru wa thamani ya mauzo wa 16% kwa mkate na ushuru wa 25% kwa mafuta ya kupikia.

Pia kulikuwa na ongezeko lililopangwa la ushuru wa miamala ya kifedha na vile vile ushuru mpya wa kila mwaka wa umiliki wa gari unaofikia 2.5% ya thamani ya gari.

Serikali ilisema inaacha hatua hizi huku kukiwa na malalamiko ya umma.

Ushuru wa eco

Ushuru wa eco, unaoelezwa kuwa ni tozo kwa bidhaa zinazochangia kuharibu mazingira, ni kifungu kingine muhimu cha muswada huo ambacho sasa serikali imependekeza kufanyiwa marekebisho.

Wakosoaji hao walieleza kuwa itasababisha kupanda kwa gharama za vitu muhimu mfano nepi na vitambaa vya sodo jambo ambalo lilionekana kuonesha kutojali maslahi ya wengi kwani wapo wasichana wengi ambao wanashindwa kumudu bidhaa hizo mara nyingi hukosa shule wakati wa siku za hedhi.

Nepi za watoto pia zingeathirika.

Kufuatia kilio, serikali ilisema ushuru huo utatumika tu kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, ikisema kuwa hilo litakuza ukuaji wa viwanda vya ndani.

Lengo lingine kuu la ushuru huu wa eco ni bidhaa za kidijitali, zikiwemo simu za mkononi, kamera na vifaa vya kurekodia pamoja na vifaa vya televisheni na redio. Kupanda kwa gharama ya bidhaa hizi kunaonekana kuwa hatari kwa ukuaji wa uchumi wa kidijitali, ambao Wakenya wengi wanautegemea kujikimu kimaisha.

Je, ni baadhi ya hatua gani ambazo hazijaguswa? Kodi kwa hospitali maalum

Muswada wa sheria ya fedha unatoa kodi ya 16% kwa bidhaa na huduma kwa matumizi ya moja kwa moja na ya kipekee katika ujenzi na utayarishaji wa vifaa vya hospitali maalum zenye uwezo wa vitanda 50.

Wakenya wengi wamekuwa na hofu kwamba hii inaweza kumaanisha gharama kubwa zaidi ya kupata huduma muhimu za afya kwa saratani, kisukari, dayalisisi ya figo au magonjwa mengine sugu.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya fedha, Kuria Kimani, amepuuzilia mbali madai kwamba "mswada huo unaleta ushuru kwa wagonjwa wa saratani" na kuyataja bungeni kama "uongo ".

Ada za juu za kuagiza bidhaa za nje

Muswada huo unapendekeza kuongeza kiwango cha ushuru wa forodha kutoka 2.5% hadi 3% ya thamani ya bidhaa, itakayolipwa na mwagizaji bandarini.

Ongezeko hilo linakuja mwaka mmoja tu baada ya kiwango hicho kupunguzwa kutoka 3.5% hadi 2.5%. Mabadiliko hayo yanatarajiwa kuleta mapato ya ziada kwa serikali lakini pia yanawezakusababisha kuongezeka kwa gharama ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Je, serikali imejibu vipi? Pamoja na kuondoa baadhi ya hatua zilizozua utata, Rais William Ruto amekiri kuwepo kwa maandamano hayo na kuahidi kuwa atafanya mazungumzo ili kutatua matatizo ya vijana ambao wako mstari wa mbele katika maandamano hayo.

Lakini hilo halijatuliza mivutano.

Kwa nini hatua hiyo haijawaridhisha waandamanaji? Licha ya kupunguzwa kwa baadhi ya hatua zilizopendekezwa, zingine zimesalia - ikiwa ni pamoja na ushuru wa juu wa uagizaji na ongezeko la tozo ya matengenezo ya barabara ambayo inatozwa kwenye mafuta.

Lakini hii pia imezua hasira ambayo imekuwa ikichemka kwa muda mrefu.

Baadhi ya Wakenya waliokasirishwa, ambao wanahisi wametozwa ushuru kupita kiasi, hawafikirii kuwa serikali imekuwa ikizingatia maswala yao.

Bw Ruto amedai kuwa ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine za Kiafrika Kenya ina kiwango cha chini cha ushuru - lakini hii haikuwashawishi wengi kutuliza hamaki zao.

Mazungumzo ya kila siku, ambayo tayari yalikuwa yametawaliwa na uchungu wa kutozwa ushuru, sasa yamefikia kilele.

Mswada wa fedha wa mwaka huu haukuwa wa kwanza ambao haukupendwa na Bw Ruto.

UIe wa mwaka jana, ambao pia ulizua maandamano, ulianzisha ushuru mwingi ambao haukupendwa na ambao mpango wa sasa unaongeza, na kuzidisha maumivu.

Waandamanaji wenye hasira wangependelea serikali kupunguza matumizi yake, kama ambavyo Wakenya wengi wamelazimika kufanya katika nyakati ngumu za kiuchumi, na kushughulikia ufujaji na ufisadi.

Serikali siku za nyuma ilisema ilikuwa itafuatilia hilo lakini imeshindwa kuwashawishi wengi kwamba imefanya vya kutosha kuzuia utumizi mbaya wa fedha za umma.

Nini kitatokea baadaye? Siku ya Jumanne, wabunge walipigia kura na kupitisha marekebisho ya serikali katika sehemu za rasimu ya sheria hiyo, ambayo iliidhinishwa na bunge wiki jana.

Muungano unaotawala una idadi ya kutosha bungeni kuruhusu mswada uliorekebishwa kupitishwa hatimaye katika wamu ifuatayo. Baada ya kupitishwa, rais atalazimika kuitia saini kuwa sheria ndani ya siku 14 au kuirejesha bungeni ikiwa na pendekezo la marekebisho zaidi.

Ingawa haiwezekani, serikali inaweza pia kuchagua hatua zingine kwa nia ya kupunguza shinikizo, pamoja na kuahirisha mswada huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: