Utaratibu wa Facebook ulisaidia kuchochea kuenea kwa chuki na vurugu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia, kesi ya kisheria inadai.
Abrham Meareg, mtoto wa mwanachuo kutoka Ethiopia aliyepigwa risasi na kuuawa baada ya kushambuliwa kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook, ni miongoni mwa waliowasilisha kesi dhidi ya Meta.
Wanataka mfuko wa $2bn (£1.6bn) kwa waathiriwa wa chuki kwenye mtandao wa Facebook na mabadiliko ya kanuni za jukwaa.
Hata hivyo kwa upande wake, Meta ilisema iliwekeza sana katika kuendesha mijadala na teknolojia ili kuondoa chuki.
Mwakilishi alisema matamshi ya chuki na uchochezi wa ghasia ni kinyume na sheria za jukwaa.
‘’Kazi yetu ya usalama na uadilifu nchini Ethiopia inaongozwa na maoni kutoka kwa mashirika ya kiraia na taasisi za kimataifa,’’ mwakilishi huyo alisema.
Hali kama njaa
Kesi hiyo, iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Kenya, inaungwa mkono na kikundi cha kampeni cha Foxglove.
Meta ina kitovu cha udhibiti wa maudhui katika mji mkuu wa Kenya Nairobi.
Mamia kwa maelfu ya watu wamefariki katika mzozo kati ya serikali ya Ethiopia na vikosi vyake katika eneo la kaskazini la Tigray, huku wengine 400,000 wakiishi katika mazingira yanayofanana na njaa.
Mwezi uliopita, makubaliano ya amani ya kushtukiza yalikubaliwa - lakini hivi majuzi, kumekuwa na ongezeko la mauaji ya kikabila kati ya jamii zinazozungumza Amhara- na Oromo.
Mwaka jana babake Bw Meareg alikua mmoja wa wahanga wa ghasia nchini humo.
Mnamo tarehe 3 Novemba 2021, Prof Meareg Amare Abrha alifuatwa nyumbani kutoka chuo kikuu chake na watu waliokuwa wamejihami kwa pikipiki na kufyatuliwa risasi karibu wakijaribu kuingia nyumbani kwa familia hiyo.