Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ethiopia yatangaza mazungumzo ya amani na kundi la waasi la Oromo

Ethiopia Yatangaza Mazungumzo Ya Amani Na Kundi La Waasi La Oromo Ethiopia yatangaza mazungumzo ya amani na kundi la waasi la Oromo

Mon, 24 Apr 2023 Chanzo: Bbc

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed siku ya Jumapili alisema serikali yake imeanzisha mazungumzo na kundi la Oromo Liberation Army (OLA), linalohudumu katika eneo la Oromia, eneo kubwa na lenye watu wengi zaidi nchini humo.

"Mazungumzo na Oneg Shene yataanza siku moja baada ya kesho nchini Tanzania," Bw Abiy alisema, akitumia jina jingine la OLA.

Alisema "serikali ya Ethiopia na watu wanahitaji sana mchakato huu wa mazungumzo," akiongeza, "Ninatoa wito kwa vikundi vyote kutekeleza jukumu (lao)."

Bw Abiy alisema hayo katika hotuba ya kusherehekea mkataba wa amani ambao serikali yake ilitia saini na chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) mwezi Novemba, ili kumaliza vita huko Tigray.

Hakutoa maelezo zaidi juu ya muundo na wapatanishi wa mazungumzo hayo.Hata hivyo, alitoa wito kwa pande zote "kukumbuka kwamba hatufaidiki chochote kutokana na vita".

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, OLA ilithibitisha mazungumzo hayo ikisema ni "hatua muhimu na chanya kuelekea kuanzishwa kwa amani ya kudumu katika eneo hilo".

Ilisema serikali imekubali masharti yake ya mazungumzo ya amani, ikiwa ni pamoja na kujumuisha "mpatanishi wa upande wa tatu".

OLA na serikali ya shirikisho hulaumiana kwa mashambulizi kadhaa katika eneo la Oromia.

Kundi hilo la waasi, ambalo linadai kupigania haki za watu wa kabila la Oromo, lilitangazwa kuwa kundi la kigaidi na serikali ya shirikisho mnamo Mei 2021.

Mzozo kati ya OLA na serikali ya shirikisho ni tofauti na mapigano ya Tigray, lakini OLA ilianzisha muungano na TPLF mnamo 2021.

Chanzo: Bbc