Ethiopia inawaruhusu raia wake kutumia mitandao ya Facebook, Telegram, TikTok na YouTube kwa mara ya kwanza ndani ya zaidi ya miezi mitano.
Huduma hizo zilifungiwa tarehe 9 Februari mwaka huu kufuatia mvutano kati ya Kanisa la Orthodox la Ethiopia na serikali.
Ni watu waliokuwa na uwezo wa kutumia programu ya mtandao wa kibinafsi (VPN) ndio wanaoweza kuingia kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii - ghama ilikuwa juu.
Kanisa la Orthodoxi lilikabiliwa na mgawanyiko mwezi Februari wakati baadhi ya maaskofu wakuu kutoka eneo la Oromia walisema wanataka kuunda dayosisi mpya ili kufanya ibada kwa lugha ya Kioromo.
Hatua hiyo ilisababisha mzozo mkali, lakini juhudi za upatanishi za serikali sasa zimeshughulikia mvutano huo.
Mamlaka haijatoa tamko lolote kuhusu uamuzi wa kuondoa marufuku hiyo.
Mwezi uliopita, mkuu wa Ethio Telecom alisema marufuku hiyo sio uamuzi uliochukuliwa na kampuni hiyo inayomilikiwa na serikali.
Kulingana na Jumuiya ya Mtandao, marufuku hiyo imegharimu Ethiopia takriban dola milioni 42 kwa sababu ya athari kwa biashara.
Wengine wanasema takwimu ni kubwa zaidi. Baadhi ya maeneo ya mkoa wa kaskazini wa Tigray, ambapo mzozo wa kikatili wa miaka miwili ulimalizika Novemba mwaka jana, yamesalia bila ufikiaji wa mtandao.