Serikali ya Ethiopia imeishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono kwenye masuala ya kikanda na kimataifa, ikiwamo kwenye suala la matumizi ya maji ya Mto Nile.
Kaimu Mkuu wa Itifaki wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, Balozi Alemayehu Sewagegn pia ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali ya nchi hiyo kuhakikisha changamoto za usalama zinapata ufumbuzi nchini humo.
Sewagegn alitoa pongezi hizo jana wakati Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA), Innocent Eugene Shiyo alipokuwa akiwasilisha nakala za hati za utambulisho katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.
Balozi Sewagegn alipokea nyaraka hizo kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Demeke Mekkonen.
Alimkaribisha Balozi Shiyo nchini Ethiopia na akampongeza kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini humo.
Alielezea uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Ethiopia uliojengwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Mfalme Haile Selassie ambao walifanya kazi kubwa kuanzisha Umoja wa Afrika.
Balozi Shiyo pia aliwasilisha salamu za heri kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kwa Rais wa nchi hiyo, Sahle- Work Zewde.
Alisema ziara ya Rais Sahle-Work Zewde nchini Januari mwaka huu ilikuwa na mafanikio makubwa na kueleza kuwa marais wa nchi hizo walikubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji, uchukuzi, nishati, mifugo na bidhaa za ngozi, utalii, uhamiaji na ulinzi na usalama.