Serikali ya Ethiopia imesema kuwa inakusudia kujumuisha vikosi vyote maalumu vya majimbo ya kikanda ima katika jeshi la taifa, au polisi ya shirikisho au majimbo; hatua ambayo inaweza kuhesabiwa kama mpango wa kuyapunguzia mamlaka majimbo yanayosimamia mambo yake yenyewe.
Inafaa kuashiria hapa kuwa majimbo kumi nchini Ethiopia yanajiendeshea mambo yake yenyewe, kuanzia kuwa na majeshi yao hadi haki ya kutumia lugha zao wenyewe. Serikali ya Ethiopia imebuni mpango huo ili kuwa na jeshi lenye nguvu kwa kuanza kuchukua hatua za kivitendo ambazo zitaruhusu vikosi maalumu vya wanajeshi kutoka kila jimbo kuunganishwa katika mifumo mbalimbali ya usalama. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya serikali.
Masaa machache kabla ya tangazo hili la serikali ya Addis Ababa kutolewa, duru za habari katika jimbo la Amhara ambalo ni pa pili kwa ukubwa huko Ethiopia ziliarifu kuibuka mapigano kati ya askari jeshi wa taifa wa jimbo hilo. Mapigano hayo yalijiri baada ya baadhi ya vikosi maalumu vya Amhara kukataa kusalimisha silaha zao kama sehemu ya mchakato wa kujiunga katika jeshi la taifa.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, vikosi vya Amhara vilimuunga mkono Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed dhidi ya uasi wa Wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray (TPLF) kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 2020. Hiyo haikuwa mara ya kwanza kushuhudiwa mapigano na mzozo katika jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia.