Mamlaka katika eneo linalokabiliwa na utovu wa usalama la Tigray nchini Ethiopia, imeonya kuhusu uwezekano wa kutokea kwa baa la njaa linalotokana na ukame na athari zinazosababishwa na mapigano ya miaka miwili katika eneo la kaskazini.
Getachew Reda, rais wa muda wa mamlaka ya Tigray, amesema zaidi ya asilimia 91 ya raia katika eneo hilo wanakabiliwa na tishio la baa la njaa na kutoa wito kwa serikali ya Ethiopia na jamii ya kimataifa kutoa msaada.
Katika taarifa iliyotumwa kwenye mtandao wa X, ambayo zamani ilijulikana kama Twitter, Getachew alifananisha hali hiyo na njaa iliyotokea nchini Ethiopia katika miaka ya 1980 ambayo ilisababisha vifo vya takriban watu milioni moja.
"Tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya Pretoria, maelfu ya raia wa Tigray wameangamia kutokana na ukosefu wa chakula," Getachew alisema, akirejelea makubaliano ya amani ya Novemba 2022 ambayo yalimaliza vita kati ya waasi wa Tigray na vikosi vya serikali ya Ethiopia.
Hali halisi inayoendelea katika vijiji vya kaskazini mwa Ethiopia haiwezi kuthibitishwa kwa uhuru kwani ufikiaji wa vyombo vya habari katika eneo la Tigray umezuiwa na serikali ya shirikisho.
Getachew aidha ameeleza kuwa kusimamishwa kwa muda kwa kwa utoaji wa misaada mapema mwaka huu na Marekani na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) pia kumechangia katika mgogoro huo.