Wakazi katika miji miwili mikubwa katika eneo la Amhara nchini Ethiopia, mji mkuu wa jimbo la Bahirdar na Gondar wa kihistoria, wameiambia BBC kwamba mapigano makali kati ya wanamgambo wa eneo hilo na wanajeshi wa serikali yameendelea Jumanne huku ghasia zikionyesha hakuna dalili ya kupungua.
Kulingana na wakazi hao utumiaji wa silaha nzito nzito umeibua wasiwasi juu ya usalama wa raia.
Kituo cha redio kinachomilikiwa na serikali huko Bahirdar kimesimamisha utangazaji, wakazi walisema.
Mapigano pia yameendelea huko Debrebirhan, kilomita 130 kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa, ambapo wakazi waliripoti kuona ndege zisizo na rubani zikipaa angani.
Wanaharakati wanaohusishwa na wanamgambo hao wanadai kudhibiti miji midogo na vijiji vingine lakini BBC haijafanikiwa kuthibitisha madai kikamilifu.
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom ambaye ni Muethiopia ameeleza wasiwasi wake juu ya ghasia zinazoendelea.
“Ni vigumu kufikia watu baada ya barabara kufungwa; mawasiliano kutatizwa kutokana na kusitishwa kwa huduma intaneti,” Dk. Tedros aliandika kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Huku hayo yakijiri kamata kamata ya watu imeendelea kuripotiwa mjini Addis Ababa huku mwandishi wa habari akiwa miongoni mwa waliozuiliwa.
Bekal Alamirew, mwanzilishi wa Alpha Media, pia alikuwa amekamatwa mwaka jana wakati wa vita vya Tigray.