Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, ameipeleka Serikali ya nchi hiyo mahakamani baada ya kudaiwa kuzuiwa kusafiri kwenda Korea Kusini kwenye mkutano.
BBC imeripoti kuwa, inadaiwa kuwa Lungu alialikwa kwenye mkutano wa amani duniani lakini alipokaribia kuondoka, alishushwa kwenye ndege yake kwa sababu hakuwa na kibali cha Serikali cha kusafiri.
Lungu sasa anatafuta mapitio ya mahakama katika Mahakama Kuu ya Lusaka, kwa mujibu wa nyaraka alizowasilisha mahakamani, anapinga uamuzi wa Serikali wa kumzuia kusafiri kwenda Korea Kusini.
Chama chake cha Patriotic Front (PF), kimelaani kitendo hico kinachodaiwa kufanywa na Serikali, kikitaja kuwa ni kinyume cha sheria.
"Ikiwa amealikwa na safari, italipiwa au anaweza kukidhi gharama za safari yake mwenyewe na ya wapambe wake, hahitaji kujuisha Serikali," amesema Emmanuel Mwamba, msemaji wa PF.
Mwamba amesema Rais huyo wa zamani, awali alizuiwa kusafiri kwa matibabu licha ya kuomba kibali kutoka katika ofisi ya Baraza la Mawaziri.
“Vitendo hivi vya kibabe na vya kidikteta ni ukiukaji wa haki za kimsingi za Rais wa zamani na hazina nafasi katika demokrasia ya kweli,” amesema.
Lungu alishindwa kwenye uchaguzi mkuu na Rais Hakainde Hichilema mwaka wa 2021. Ingawa baadaye alitangaza kustaafu siasa za moja kwa moja, hata hivyo duru za siasa nchini humo zinamtazamia kurejea na huenda akashiriki uchaguzi wa 2026.