Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imetangaza kupunguza vikwazo dhidi ya Guinea na Mali, baada ya kufanya hivyo kwa nchi ya Niger, mataifa yanayoongozwa na serikali za kijeshi.
Hatua hii ya ECOWAS inakuja baada ya nchi hizo mbili kuwekewa vikwazo vya kiuchumi mwaka 2020 na 2023 baada ya jeshi kuchukua madaraka kwenye nchi hizo.
Vikwazo vilivyoondolewa kwa nchi hizo ni vya kiuchumi, lakini pia raia wa Mali wameondolewa vizuizi vya kufanya kazi kwenye taasisi ya Jumuiya ya ECOWAS.
Mbali na kuondolewa vikwazo hivyo, ECOWAS imeendelea kuwasimamisha uanachama nchi hizo pamoja na Burkina Faso baada ya jeshi kuzipindua serikali za kiraia. Mataifa yanayoongozwa na jeshi Afrika Magharibi yalikuwa yametishia kuondoka kwenye muungano wa Ecowas
Kwa upande wa Niger, zuio la safari za ndege kwenye ukanda wa ECOWAS na kuzuiwa kwa mali ziliondolewa Jumamosi iliyopita kwa sababu za kibinadamu kwa mujibu wa jumuiya hiyo.
Wakati wa kikao cha wakuu wa ECOWAS kilichofanyika jijini Abuja, Jumamosi iliyopita, wakuu wa Jumuiya hiyo wameonesha nia ya kuanzisha tena mazungumzo na uongozi wa kijeshi nchini Mali, Niger na Burkina Faso ambazo zimetangaza kujiondoa kwenye jumuiya hiyo.