Afrika

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ecowas ‘yaingia ubaridi’ sakata la Niger

ECOWAS: Uingiliaji Wa Kijeshi Nchini Niger 'itakuwa Hatua Ya Mwisho' Ecowas ‘yaingia ubaridi’ sakata la Niger

Mon, 28 Aug 2023 Chanzo: mwanachidigital

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) imesitisha mpango wake wa kuliingilia kijeshi Taifa la Niger, na kuona badala yake ifanye suluhisho la kidiplomasia.

Taifa hilo linalopatikana Afrika Magharibi, linapitia misukosuko ikiwemo vikwazo kutoka Ecowas tangu Julai 26, baada ya jeshi la nchi hiyo kumuondoa Rais aliyekuwa madarakani Mohamed Bazoum.

Awali kulikuwa na mpango wa Jumuiya hiyo kuiingilia kijeshi Niger taarifa zilizokuwa zinaongeza vuguvugu ya uwezekano wa kutokea vita katika ukanda wa Sahel.

Kwa mujibu wa tovuti ya The East African, mwishoni mwa wiki, Rais wa Nigeria Bola Tinubu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ecowas, aliashiria kutafuta usuluhishi wa kidiplomasia.

Naye Abdulsalami Abubakar, mjumbe maalum wa Ecowas kuhusu mkwamo wa kisiasa wa Niger, alitangaza suluhu ya kidiplomasia inaweza kufikiwa kuhusu mzozo ambao umeikumba nchi hiyo.

Abubakar aliwaambia waandishi wa habari kwamba majadiliano na jeshi la nchi hiyo yameonyesha dalili nzuri.

"Lazima niseme kwamba ziara yetu nchini Niger imekuwa na matunda mengi na kwamba imefungua njia ya kuanza kuzungumza, na tunatumai, tutafika mahali," alisema Abubakar baada ya kuwasilisha ripoti kuhusu hali hiyo kwa Rais Tinubu.

Abubakar aliongoza ujumbe maalum wa Ecowas ili kushughulikia mkwamo wa kijamii na kisiasa. Ecowas imesema Serikali ya kijeshi inabidi irejeshe mamlaka kwa Rais Bazoum.

Chanzo: mwanachidigital