Umoja wa Ulaya (EU) umeelezea wasiwasi wake kuhusu Bunge la Uganda kupitisha mswada wa kupinga mapenzi ya jinsia moja.
Katika taarifa yake, EU ilisema kuwa inapinga hukumu ya kifo katika hali zote.
Imeongeza kuwa kuharamishwa kwa mahusiano ya jinsia moja ni kinyume na sheria za kimataifa za haki za binadamu.
"Umoja wa Ulaya utaendelea kushirikiana na mamlaka ya Uganda na mashirika ya kiraia ili kuhakikisha kwamba watu wote, bila kujali mwelekeo wao wa kijinsia na utambulisho wa kijinsia, wanahudumiwa kwa usawa, kwa utu na heshima," taarifa hiyo iliendelea kusema.
Siku ya Jumanne, Wabunge wa Uganda walipitisha sheria ambayo inafanya kuwa haramu kutambuliwa kama LGBTQ, na ambayo inaagiza adhabu ya kifo katika kesi za unyanyasaji wa watoto wa jinsia moja au shambulio dhidi ya watu wengine walio hatarini.
Pia inaweka maisha ya kifungo kwa biashara ya watoto kwa madhumuni ya kuwahusisha watoto katika vitendo vya ushoga.
Siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema kuwa sheria hiyo mpya iliyopitishwa inakwenda kinyume na haki za kimsingi za binadamu na kuitaka serikali kutazama upya utekelezaji wake.
Wanaharakati wa mashinani na mashirika ya haki za binadamu yamehoji kuwa sheria ina uwezekano wa kuwa na athari zaidi ya watu wanaojitambulisha kuwa wachache wa kingono, na kuathiri maeneo kama vile vyombo vya habari, utoaji wa huduma za afya na haki ya faragha.
Mswada huo hauwi sheria ya uendeshaji hadi Rais Yoweri Museveni atakapoutia saini.